Maoni ya Wahariri wa Magazeti ya Ujerumani | NRS-Import | DW | 30.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Maoni ya Wahariri wa Magazeti ya Ujerumani

Amri iliyotolewa na Trump kuwapiga marufuku raia kutoka nchi saba wasiingie nchini humo, na uteuzi wa Martin Schulz kugombea ukansela wa Ujerumani, ni mada zilizohanikiza katika magazeti ya Ujerumani leo. (30.01.2017)

Maandamano ya kuipinga amri iliyotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump, kuwafungia milango raia kutoka Iraq, Syria, Iran, Sudan, Libya, Somalia na Yemen, yanaendelea katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, huku Wamarekani wakionyesha mshikamano na wale walioathiriwa moja kwa moja na agizo hilo. Mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung la mjini Mainz alisema hatua hii, haijawaathiri asilimia kati ya 90 na 99 ya waisilamu wenye misimamo mikali ya kidini wala propaganda ya kundi linalojiita dola la kiislamu, IS. Agizo hilo limeiacha nje Saudi Arabia, nchi walikotokea washukiwa wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Mhariri alisema kwa kundi la IS vita kati ya tamaduni vitahakikisha linaendelea kuimarika. Hatua hiyo haimsaidii sana Trump, kwa mfano kwa ukweli uliodhihirika kwamba mahakama hazikumuunga mkono na baadhi ya wanachama wa chama chake cha Republican katika bunge la Marekani hawako tayari kuyaunga mkono kila mageuzi anayotaka kuyafanya kupitia amri anazotia saini kama rais.

Gazeti la Hannoverscher Allgemeine kuhusu suala la Trump liliandika: Trump amekiuka katiba kwa marufuku yake dhidi ya waislamu kuingia Marekani. Anaigawa jamii ya kisasa na anaifanya dunia kukabiliwa na hatari zaidi kuliko ilivyokuwa kabla yeye kuingia madarakani, huku akijinasibu kama mlinzi wa taifa kwa wapiga kura waliomuunga mkono. Waislamu wenye misimamo mikali wamepata kitu cha kukabiliana nacho nchini Marekani na hata Mashariki ya Kati. Hili ni suala ambalo vyombo vya usalama vimekuwa vikijitahidi kuliepusha.

USA Amerika protestiert gegen den Einreiseverbot für Muslime Miami (Getty Images/J. Raedle)

Maandamano ya kupinga agizo la rais Trump

Mhariri alitilia maanani kwamba ulimwengu sharti uendelee kujitolea kwa dhati katika vita dhidi ya ugaidi kwa kushughulikia masuala muhimu na kuweka mipaka kati ya wahalifu na migogoro ya kimahakama. Ikiwa Trump ndiye msitari unaosababisha mgawanyiko kwa misingi ya dini, hilo linakuwa suala kubwa. Kwani anatia moto kati kiberiti cha ulimwengu huu, aliandika mhariri wa gazeti hilo.

Schulz ateuliwa kugombea ukansela

Chama cha Social Democtratic, SPD, kimemteua rasmi Martin Schulz kuwania nafasi ya ukansela katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu. Mhariri wa gazeti la Scwäbische Zeitung la mjini Ravensburg katika maoni yake alisema chama hicho kina sababu nyingine ya kusherehekea. Na kwa kuwa hilo ni nadra kutokea, basi kimesheherekea kwa namna ya kipee kabisa.

Martin Schulz ameikonga mioyo ya wanachama wa chama cha SPD katika hotuba yake ya kukubali uteuzi wa chama chake. Alileta mwamko mpya ambao chama iliukosa chini ya mwenyekiti aliyeondoka, Sigmar Gabriel. Schulz alitoa mwito watu wa kawaida wa tabaka la chini waheshimiwe na wapate haki, tabaka ambalo yeye mwenyewe anatokoea.

Berlin SPD PK Martin Schulz Kanzlerkandidatur (Reuters/H. Hanschke)

Martin Schulz

Mhariri wa gazeti hilo aidha alisema licha ya Schulz kushikilia nafasi ya spika wa bunge la Ulaya kwa miaka mingi, ameonyesha unyenyekevu zaidi kuliko wanasiasa wengine. Na kwa namna hiyo anayabeba matumaini ya chama cha SPD. Fauka ya hayo, mhariri anasema, ana kibarua kipevu kinachomkabili mbele yake kwani chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, kinaonekana na wengi kama chama kinachofuata siasa za wastani za mrengo wa shoto, na kwa hiyo panabakia nafasi ndogo sana kwa chama cha SPD.

Schulz ana kazi ngumu

Kwa kuwa Schulz anaweza kufaulu kuwa kansela, huenda akalazimika kushirikiana na Sahra Wagenknecht wa chama cha siasa kali za mrengo wa shoto cha Die Linke, anayetaka Ujerumani ijiondoe kutoka kwa jumuiya ya kujihami ya NATO. Mshirika mwingine anaweza kuwa chama cha Kijani ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikiegemea upande wa chama cha CDU. Lakini hata hivyo Schulz amefaulu kukisogeza mbele chama cha SPD.

Gazeti la Der neue Tag liliandika kuhusu uteuzi wa Schulz liliandika: Schulz amedhihirisha umahiri wake kisiasa katika bunge la Ulaya zaidi ya mara moja. Mnamo 2003 wakati waziri mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, alipompendekezea Schulz achukue jukumu kama manusura wa kambi ya mateso ya enzi ya utawala wa manazi kwenye filamu, Schulz hakuonyesha hasira bali alitulia na kunyamaa kimya. Au mwezi Machi 2016, wakati yeye kama spika wa bunge la Ulaya, alipomteua naibu spika kutoka kwa chama cha mrengo wa kulia cha Ugiriki, Golden Dawn, kwa sababu alikuwa ametoa kauli za kibaguzi dhidi ya Waturuki. Schulz ni mtu mwenye stahamala, anaelewa jinsi ya kukaa na watu na kama mgombea ameshaanza kupasha moto misuli kwa kinyang'anyiro cha ukansela.

Mwandishi:Josephat Charo/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com