Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 09.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Mada iliyohanikiza katika maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo (09.10.2012) ni ziara ya kansela Angela Merkel nchini Ugiriki. Vile vile wamezungumzia kuhusu mfuko wa kudumu wa uokozi wa Umoja wa Ulaya, ESM.

epa03426406 Greek Prime Minister Antonis Samaras (R) welcomes German Chancellor Angela Merkel (L) at Athens International Airport, Greece, 09 October 2012. German Chancellor Angela Merkel travelled to Greece for talks with leaders eager for her support to avoid bankruptcy and remain in the eurozone as angry Greeks prepare to protest against her austerity drive. EPA/PANTELIS SAITAS pixel

Griechenland Angela Merkel Ankunft in Athen mit Antonis Samaras

Kuhusu ziara ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Ugiriki, gazeti la Neue Presse linasema ziara hiyo katika mji mkuu Athens, imechelewa sana kwani kiongozi huyo alifanya ziara yake ya mwisho nchini humo kabla kuibuka mzozo wa madeni. Mhariri wa gazeti hilo anasema leo hii kansela Merkel anatakiwa kutambua juhudi zilizofanywa na Wagiriki kwa heshima ile ile inayostahiki umma wa taifa hilo. Pia anasema ziara hii haihusiani na kuwahimiza watie bidii.

Mhariri anatilia maanani kwamba kansela Merkel hapaswi hata kidogo kujionyesha kama mwalimu mkuu au msimamizi mkuu wa kanda inayotumia sarafu ya Euro, kwani Ujerumani haina jukumu hili barani Ulaya, hata kama serikali ya Ujerumani mara kwa mara hufanya kana kwamba bara la Ulaya linalazimika kufuata kanuni zake na sheria kuhusu masuala ya fedha.

Gazeti la Neue Presse linasema sasa Merkel anaweza kutoa ishara nzuri ya umuhimu mkubwa kwamba Ujerumani inaiunga mkono kikamilifu sarafu ya Euro na Ugiriki. Ufanisi mkubwa wa ziara yake utapatikana kama Merkel atawapelekea kitu Ugiriki, kwa mfano muda zaidi kwa Wagiriki kutekeleza mpango wao wa kufunga mkaja.

Merkel abebe zawadi

Nalo gazeti la Berliner Morgen kuhusu ziara hiyo ya Merkel Ugiriki linasema kama kiongozi huyo hataki kupata aibu au kuvunjika moyo kutokana na ziara hii, basi lazima abebe kijizawadi kidogo kwa ajili ya wenyeji wake katika mkoba wake; bila kuondoa uwezekano kwamba wazo hili alikuwa nalo.

Gazeti linazungumzia kauli ya waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, kuwa ziara hii si ishara kwamba Ugiriki itapatiwa awamu nyingine ya mkopo, bali inalenga kuhakikisha masuala ya kifedha na kiuchumi yamekaa sawa ili nchi hiyo iweze kujisimamia yenyewe kuanzia mwaka 2020. Mhariri anauliza, je, waziri huyu muhimu katika serikali ya Merkel anaweza kutoa kauli hiyo bila kuwa na wasiwasi wa kupigwa kiboko na bosi wake?

Mfuko wa Uokozi Ulaya

Mada ya pili iliyozingatiwa na wahariri leo inahusu mfuko wa kudumu wa uokozi wa Umoja wa Ulaya, ESM. Gazeti la Saarbrücker Zeitung linasema kuanzishwa rasmi kwa mfuko huo ni hatua kubwa ya milenia kwa bara la Ulaya.

Mhariri wa gazeti hilo anasema imetabiriwa kwamba mfuko huo huenda utatumiwa kuiangamiza sarafu ya Euro na hata kuinyonya Ujerumani, lakini ukweli ni kwamba kufikia sasa serikali ya Ujerumani imepata faida tu kwa kushiriki juhudi za kuutanzua mzozo wa madeni Ulaya. Ujerumani inanufaika sio tu kutokana na riba bali pia uwekezaji inayougharamia. Ujerumani ambayo inashikilia nafasi ya pili katika uuzaji wa bidhaa katika nchi za nje, hunufaika inapotoa.

Mwandishi: Josephat Charo/DPA/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman