1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMashariki ya Kati

Mamilioni ya waislamu wauwanza mwezi mtukufu wa Ramadhani

Amina Mjahid
23 Machi 2023

Waumini wa dini ya kiislamu wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mamilioni ya waumini hao wameingia katika kipindi hiki muhimu cha maombi kwa matumaini ya kupatikana amani katika mataifa yaliyo kwenye migogoro

https://p.dw.com/p/4P6zP
Saudi-Arabien | Masjid al-Haram Moschee in Mecca
Picha: Hani Alshaer/AA/picture alliance

Waislamu wameingia katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, wakati mataifa kadhaa na serikali Mashariki ya kati zikichukua hatua kujaribu kutuliza migogoro inayoendelea kutanuka kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na janga la matetemeko ya ardhi yaliyotokea Uturuki na Syria mapema mwezi uliopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50,000.

Ndani ya wiki nne zijazo, mamilioni ya waislamu watajinyima kula na kunywa kuanzia mapema alfajiri hadi jioni. Kulingana na dini ya kiislamu kufunga katika mwezi huu mtukufu kunakusogeza karibu na mungu wako na kukukumbusha ugumu unaowapata masikini au watu wasio na uwezo wa kujimudu kimaisha.

Waislamu duniani waanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan

Kando na kufunga ndani ya mwezi huu mtukufu, Sadaqa ambayo ni moja ya nguzo tano za uislamu, inahimizwa kutolewa na ndio maana katika misikiti mingi vyakula huwa vinatolewa kwa wasioweza kupata riziki mwezi huu. Hata hivyo kwa taifa kama Sudan mwezi huu umekuja wakati kukiwa na ahadi ya kurasa mpya katika siasa za taifa hilo la Afrika. Sudan ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu serikali ya muungano ilipoondolewa kupitia mapinduzi ya kijeshi Oktoba mwaka 2021.

Na sasa kuna matumaini ya serikali mpya ya mpito, kuundwa kabla ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani kama walivyoahidi watawala wa kijeshi na wadau wengine wa kisiasa nchini humo. Lakini Wasudan wengi hawana matumaini ya hilo kutokea, wengi wanalalamika juu ya kupanda kwa gharama ya maisha.

Kupanda kwa bei za bidhaa kunavuruga hali ndani ya mwezi  mtukufu

Mali | Moschee in Djenne
Wanunuzi wakiwa ndani ya soko moja nje ya msikiti uliopo mjini Djenne, Mali Picha: Michel Renaudeau/IMAGO

Kwengineko nchini Israel na eneo la Palestina viongozi huko waliahidi kutuliza mivutano yao wakati mwezi wa Ramadhani unapowadia, mivutano inayotokana na miezi kadhaa ya mapigano katika eneo la ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem.

Kuanzia Gaza hadi Khartoum, Tunisia hadi Sanaa kuongezeka kwa bei za bidhaa kunaelezea wazi changamoto inayowakumba raia huko ambako vita vimesambaratisha hali ya maisha. Mataifa ya kiarabu yanaendelea kuathirika kufuatia uchumi kuyumba kutokana na vita vya Ukraine kufuatia mataifa mengi kutegemea nafaka kutoka Mashariki mwa Ulaya.

Ramadhani yaanza huku kukiwa na kupanda kwa bei za vyakula na nishati

Hali kusini mwa Uturuki na Kaskazini Mgharibi mwa Syria pia sio shwari kufuatia matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyopiga maeneo hayo mwanzoni mwa mwezi Februari. Familia nyingi bado hazina uwezo wa kujitayarisha kikamilifu kuupokea mwezi mtukufu wa ramadhani. Wengi wanaishi nje kwenye baridi na kukosa uwezo wa kuendelea na maisha yao baada ya janga hilo. 

Chanzo: afp/ap