Malta yawashikilia wahamiaji walioteka meli | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Malta yawashikilia wahamiaji walioteka meli

Kikosi maalumu cha jeshi la Malta kimechukua udhibiti wa meli ya mizigo iliyotekwa na wahamiaji waliiookolewa na meli hiyo katika pwani ya Libya. Wahamiaji hao wameingia Malta na watatiwa kizuizini kwa uchunguzi zaidi.

Picha zilizotolewa muda mfupi uliopita zimeonyesha wahamiaji wanne wakiwa wamefungwa pingu na kusindikizwa na polisi kutoka kwenye meli hiyo iliyotekwa. Meli hiyo imewasili Malta mapema hii leo ikiwa na wahamiaji zaidi ya 100. Picha zinaonyesha wanajeshi wenye silaha wakiwa bandarini, lakini pia kukiwa na malori yanayosubiri kuwachukua wahamiaji na kuwapeleka mahabusu.

Wahamiaji hao wanne waliofungwa pingu ndio wanaohisiwa kuwa vinara wa tukio hilo.

Meli hiyo ya mizigo Elhiblu 1 ya Uturuki iliwaokoa wahamiaji 108 ambao ni pamoja na wanawake na watoto waliokuwa wakitokea Libya kuelekea Ulaya ambao waliiteka baada ya kugundua kuwa ilikuwa inawarejesha Libya.

Kulingana na jeshi la Malta, nahodha wa meli hiyo alianza kuwasiliana na jeshi la Malta wakati meli hiyo ikiwa umbali wa maili 30 kutokea bandari ya Malta, na kuwaambia kwamba hakuwa anaioongoza meli hiyo kwa kuwa yeye na wafanyakazi wenzake walilazimishwa na kutishwa na wahamiaji kuielekeza meli hiyo hadi Malta.

Malta Valetta Flüchtlinge auf gekapertem Handelsschiff Elhiblu I (Reuters/D.Z. Lupi)

Meli ya El Hiblu. 1 baada ya kuokolewa mikononi mwa wahamiaji waliookolewa pwani ya Libya.

Jeshi hilo limesema, moja ya boti zake za doria iliizuia meli hiyo kuingia kwenye maji ya Malta na kutuma kikosi maalumu cha operesheni kilichoingia kwenye meli hiyo na kuiokoa kutoka mikononi mwa wahamiaji hao. Kikosi hicho pia kilisindikizwa na manowari mbili za kijeshi, boti nyingine ya doria na helikopta.

Hatimaye meli hiyo ilisindikizwa hadi bandari ya Valletta na kukabidhiwa kwa polisi ya Malta kwa ajili ya uchunguzi wa kina, na hakukua na taarifa zaidi iliyotolewa kuhusiana na hali ya meli hiyo.

Naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini, ambaye ana misimamo mikali dhidi ya wahamiaji alisema Italia isingekubali kuikaribisha meli hiyo bandari zake na kuwafungulia milango wahamiaji hao aliowaita wahalifu kutokana na kitendo hicho cha uharamia.

Italien Parlament in Rom | Matteo Salvini, Innenminister (Reuters/Y. Nardi)

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Matteo Salvini anapinga vikali wahamiaji

Kutokana na misimamo hiyo mikali ya Italia dhidi ya wahamiaji, boti zinazowaokoa katika bahari ya Mediterania huwarejesha Libya.

Meli hiyo iliwaokoa wahamiaji waliokuwa wamekwama kwenye eneo la maji ambako walinzi wa pwani ya Libya wanahusika nalo na kuanza kurejea Tripoli. Hata hivyo meli hiyo ghafla ilibadilisha mwelekeo ikiwa umbali wa maili sita hadi bandarini na kuanza kuelekea upande wa Ulaya.

Kulingana na Umoja wa Mataifa na makundi ya misaada, wahamiaji wanaotokea Libya, taifa lililokumbwa na machafuko wanakabiliwa na visa vya mateso, utekwaji, biashara haramu ya binadamu.

Umoja wa Ulaya hapo jana umetangaza kusitisha kuepeleka meli za doria ambazo zimekuwa zikiwaokoa maelfu ya wahamiaji wanaopitia bahari ya Mediterania kuingia nchi za Ulaya, na kuwapeleka Italia. Hata hivyo idadi ya wahamiaji wanaotoka Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati inatajwa kupungua kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2015, wakati Ulaya ilipokabiliwa na mzozo wa wahamiaji ambao haukuwahi kushuhudiwa tangu vita vya pili vya dunia.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE

Mhariri: Gakuba, Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com