Mahakama: Marufuku ya kutofunika nyuso Hong Kong ni batili | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mahakama: Marufuku ya kutofunika nyuso Hong Kong ni batili

Mahakama mjini Hong Kong leo imeamua kuwa amri tata ya kutofunika nyuso kwa kutumia barakoa wakati wa maandamano ni kinyume na katiba.

Uamuzi huo wa mahakama unakuja baada ya makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji mwishoni mwa juma.

Kulingana na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kituo cha radio cha Hong Kong, Mahakama ya mji huo imeabaini marufuku hiyo iliyotangazwa chini ya sheria za dharura inakiuka sheria ya msingi na inazuia haki za raia bila sababu ya msingi.

Majaji wawili, Godfrey Lam na Anderson Chow, wamesema utekelezaji wa marufuku hiyo unashindwa kuweka uzani kati ya haki za raia zinazopigiwa upatu na hatua zinazochukuliwa kuzuia haki hizo.

Marufuku dhidi ya kufunika nyuso ilitangazwa mwezi Oktoba na kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam, ambaye alianisha lengo  lake kuwa ni kusaidia kukabiliana na maandamano ya vurgu yanayoukumba mji huo kwa muda wa miezi kadhaa sasa.

Waandamanaji wamekuwa wakikaidi amri ya kutofunika nyuso

Barakoa au vifunika nyuso vimekuwa vikivaliwa na waandamanaji ili kuzuia kutambuliwa pamoja na sababu za kiusalama kutokana na polisi kutumia kila wakati mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kuwatawanya  waandamanaji.

Amri hiyo ilihuishwa kutoka sheria ya hali ya hatari wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza na waandamanaji wengi walikaidi kuitekeleza.

Mwanaharakati mashuhuri wa demokrasia mjini Hong Kong, Joshua Wong ameutaja uamuzi wa leo wa mahakama kuwa "ushindi wa nadra wa kisheria kwa waandamanaji."

Kuondolewa kwa marufuku ya kufunika nyuso kunakuja baada ya makabiliano makali kati ya waandamanaji na polisi mwishoni mwa juma.

Polisi mjini Hong Kong leo wamekivamia Chuo Kikuu kilichokuwa kikidhibitiwa na waandamanaji baada ya kushindwa usiku kucha kuingia kwenye eneo hilo.

Miale ya moto iliyotokana na mfululizo wa milipuko ilionekana kutoka ndani ya majengo pindi maaafisa wa polisi wa kutuliza fujo walipoingia kwenye viunga vya chuo hicho mapema leo alfajiri.

Waandamanaji watumia silaha za jadi kujihami

Kabla ya usiku wa manane, polisi walifyetua mara kadhaa mabomu ya kutoa machozi pamoja na warushia waandamanaji maji ya kuwasha nje ya majengo ya chuo kikuu hicho.

Kwa siku kadhaa waandamamanaji wanaoipinga serikali walijifungia ndani ya chuo kikuu cha masuala ya ufundi mjini Hong Kong wakipambana kwa kutumia mabomu ya kutengenezwa kwa mafuta pamoja na silaha za jadi.

Kwa mujibu wa polisi waandamanaji walivurumisha mabomu ya kutengenezwa kienyeji na kuchoma moto miundombinu kadhaa.

Machafuko yameongezeka mjini Hong Kong katika wiki za karibuni baada ya waandaaji wa maandamano kuwatolea wito waandamnanaji kufanya vurugu za kiwango cha juu.

Maandamano ya umma mjini Hong Kong ya kudai demokrasia yalianza kama upinzani dhidi ya sheria tata ya kupeleka wahalifu upande wa China Bara na tangu wakati huo maandamano hayo yamegeuka kuwa madai ya kufanyika mageuzi mapana ya kidemokrasia na uchunguzi huru kuhusu unyanyasaji wa polisi.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com