Maelfu wahudhuria misa iliyoongozwa na Papa Francis Bangladesh | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maelfu wahudhuria misa iliyoongozwa na Papa Francis Bangladesh

Maelfu ya wakristo na waumini wa dini nyingine, leo walikusanyika katika mji mkuu wa  Bangladesh, Dhaka, katika misa ya wazi iliyoongozwa na Papa Francis. 

Katika misa hiyo, pamoja na kuhimiza amani, Papa aliwatawaza mapadri 16.

Ziara yake ililenga kwa kiasi kikubwa katika jamii ya Wakatoliki, katika nchi hiyo, iliyo Kusini mwa Asia. Aliwashukuru wakazi hao  waliosafiri kutoka pembe mbalimbali za nchi hiyo ili kushiriki katika misa hiyo.

"Hii inaonyesha upendo mlio nao kwa kanisa," aliwaambia huku akiwahimiza kuwaombea mapadri waliotawazwa. Kadhalika, baada ya kuwasimika mapadre hao, Papa aliwaambia akisema.

"Sasa wapendwa mnatakiwa kukua katika miongozo ya kipadri, kwa nafasi yenu, mtatimiza  wajibu mtakatifu wa kufundisha katika jina la Yesu, Kristo Mwalimu. Toeni kwa furaha maneno ya Mungu mliyopokea, kwa kila mmoja."

Maelfu ya watu walionekana wakiwa wamepanga foleni katika mlango wa kuingilia katika eneo  Suhrawardy Udyan, lililo mkabala  na Chuo Kikuu cha Dhaka, ambapo misa ilifanyika chini ya ulinzi mkali.

Papa aliendeshwa kuzunguka eneo hilo, akiwa katika gari la wazi la kipapa, huku akiwapungia...... halaiki  ya watu iliyojaa katika eneo hilo.Maelfu ya watu waliendelea kumiminika hata baada ya misa kuanza.

Akizungumzia ujio huo wa Papa, mtalaamu wa masuala ya kibenki wa nchini Bangladesh Joyel Kumar alisema:

´`Ziara ya Papa itakuwa ni msaada mkubwa kwa watu wote. Itatuweka pamoja na matatizo katika jamii yatatatuliwa. Kwa wakristo wa Bangladesh, ilikuwa ni jambo zuri kwetu na tuna imaini watu wetu wakristo watatiwa moyo na hili.``

Zaidi ya 100,000 wahudhuria misa iliyoongozwa na Papa

Jumuiya  ya Wakristo Bangladesh, wanakadiria kuwa zaidi ya watu laki moja walijumuika katika misa hiyo.

Baada ya misa hiyo, Papa anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Hasina baadaye leo na kisha atajumuika katika misa inayojumuisha waumini wa dini mbalimbali, kwa ajili ya kuombea amani.

Mwakilishi wa madhehebu ya Waislamu, Hindu, Buddha na Wakristo wanatarajiwa kujumuika katika sala hiyo ambayo itafanyika katika bustani ya makazi ya askofu mkuu huyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kamati ya Kuratibu vyombo vya habari, Komol Koraiya, alilimbia shirika la habari la DPA na kusema timu ya watu 18, Warohingya wa kiislamu, ambao walikimbia machafuko Myanmar, watajumuika katika sala hiyo jioni leo.

Baada ya kufika Dhaka jana, Papa alizitaka jumuiya ya kimataifa, kuchukua hatua za dhati ili kutatua mgogoro huo wa wakimbizi kati ya Bangladesh na Myanmar.

Zaidi ya Warohingya laki sita, walikimbilia Bangladesh tangu machafuko baina ya wanajeshi na kundi hilo, kuanza Myanmar, Agosti mwaka huu.

 Awali, akiwa Myanmar  Papa alisisitiza kuimarishwa kwa amani lakini  aliepuka kutumia neno Warohingya, katika kuwaelezea wakimbizi hao.

Mamia ya vijiji vya Warohingya vilichomwa moto na wakimbizi hao waliokimbilia Bangladesh walisimulia visa vya mauji na kubakwa.

Mwandishi: Florence Majani(Dpa, Reuters)

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com