1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Ujerumani kupinga TTIP na CETA

17 Septemba 2016

Waandamanaji wameingia barabarani nchini kote Ujerumani Jumamosi (17.09.2016) kupinga mpango mkubwa sana wa kibiashara kati ya Ulaya na Marekani na hiyo kuwa pigo jipya kwa mpango huo unnaopingwa.

https://p.dw.com/p/1K4Ez
Picha: Reuters/F. Bensch

Waandamanaji wameingia barabarani nchini kote Ujerumani Jumamosi (17.09.2016) kupinga mpango mkubwa sana wa kibiashara kati ya Ulaya na Marekani na hiyo kuwa pigo jipya kwa mpango huo unnaopingwa.

Umma wa watu umemiminika mjini Berlin halikadhalika Munich licha ya kunyesha kwa mvua wakibeba mabango yenye kuwakilisha makundi kadhaa yanayopinga utandawazi, mashirika yasio ya kiserikali,vyama vya kisiasa na vyama vya wafanyakazi.

Roland Suess kutoka kundi lenye kupinga utandawazi la Attac ameliambia shirika la habari la AFP kwamba walikuwa wakitarajia watu 250,000 kujitokeza katika miji mikubwa ya Ujerumani ambapo 80,000 wanatazamiwa kujitokeza Berlin.Washiriki wamekuwa na mabango yenye kudai "demokrasia badala ya TTIP" na "kugawana na sio kugawa".

Umoja wa Ulaya na Marekani zilianza kujadili mpango huo wa Biashara na Uwekezaji kati ya Ulaya na Marekani (TTIP) hapo mwaka 2013 kwa lengo la kuanzisha soko huru kubwa kabisa la biashara duniani lenye walaji milioni 850.Duru mpya mazungumzo inatarajiwa kuanza mwezi wa Oktoba na Rais Barack Obama wa Marekani anataka makubaliano yafikiwe kabla ya kuondoka madarakani hapo mwezi wa Januari.

Mkataba mwengine mdogo kama huo kati ya Ulaya na Canada ujulikanao kwa jina la CETA  pia unaendelea kushughulikiwa na unatarajiwa kutiwa saini hapo mwezi wa Oktoba.Wafanyabiashara wenye kusafirisha nje bidhaa zao wanauunga mkono mkataba huo kwa kuwa umeahidi ushuru mdogo ,kupunguza urasimu na kutanuwa wigo wa walaji kwa bidhaa zao.

Upinzani Ulaya

Wananchi walioandamana Köln kupinga makubaliano ya TIP und Ceta.
Wananchi walioandamana Köln kupinga makubaliano ya TIP und Ceta.Picha: DW/J. D. Walter

Lakini wajumbe katika mazungumzo hayo wamekabiliwa na upinzani Ulaya ambapo walaji wamekuwa wakihofu kwamba kutaathiri soko la ajira la nchi wanachama 28 wa umoja huo na viwango vya mazingira jambo litakalopelekea upunguzaji wa gharama ambao nao utasababisha kupotezwa kwa ajira.

Suala jengine tata ni mpango wa kuanzisha mahakama maalum kusikiliza kesi zinazowasilishwa na kampuni dhidi ya hatua za serikali kukiuka masuala ya miundo jambo ambalo wanaoupinga mkataba huo wanasema inawapa makampuni kura ya turufu dhidi ya sera za serikali

Jennifer Morgan mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Greenpeace amesema "CETA na TTIP inatishia ulinzi wa mazingira na walaji kwa mamilioni ya watu barani Ulaya na Amerika Kaskazini."

Sio wananchi tu wanatofautiana

Naibu Kansela Sigmar Gabriel.
Naibu Kansela Sigmar Gabriel.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Sio tu watu wa Ulaya waliogawika kuhusu makubaliano hayo yanayopendekezwa hata serikali nazo zinatafautiana.Serikali ya Ufaransa imeweka upinzani mkali ambapo Waziri Mkuu Manuel Walls akidai kukomeshwa kwa mazungumzo hayo wakati kiongozi wa taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameelezea kuunga mkono makubaliano hayo.

Katika mahojiano ya hivi karibuni Merkel ametaja suala la kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya ambapo amesema : "tunapaswa kufanya kila tunachoweza kuzalisha ajira ......makubaliano ya biashara huru ni sehemu ya jambo hilo."

Lakini hata ndani ya serikali ya mseto kuna upinzani kwa makubaliano hayo yanayopendekezwa ambapo Naibu Kansela wa chama cha SPD mwezi uliopita ametangaza mazungumzo hayo ya TTIP " ni kama vile yameshindwa."Sigmar Gabriel ambaye ni waziri wa uchumi pia amesisitiza kwamba watu wa Ulaya lazima wasikubali kuridhia madai ya Wamarekani.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni wa taasisi ya Ipsos asilimia 28 ya wale walioulizwa wana mashaka iwapo biashara huru inaweza kuwa na manufaa.Zaidi ya nusu yaani aslimia 52 wanasema itasababisha viwango dhaifu na kuongeza bidhaa zizizokuwa na ubora.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Sudi Mnette