1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Macron yuko China kuishinikiza kusaidia amani nchini Ukraine

Lilian Mtono
5 Aprili 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini China ambako pamoja na mengineyo analenga kulishawishi taifa hilo mshirika wa Urusi, kusaidia juhudi za kuleta amani katika mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4PiPt
Indonesien | G20-Gipfel | Emmanuel Macron und Xi Jinping
Rais Emmanuel Macron akipeana mkono na rais Xi Jinping wa China kabla ya mkutano wa Musa Dua huko Indonesia, Novemba 15,2022.Picha: Ludovic Marin/Pool/AFP/Getty Images

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aidha anataraji kuirai China kuacha kuisaidia Urusi kwa silaha. Macron yuko China wakati rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa nchini Poland kwa ziara rasmi ya kikazi kwa mshirika wake huyo ambaye amesaidia pakubwa kuyahamasisha mataifa ya magharibi kumsaidia jirani yake kijeshi na hata kisiasa. 

Rais Emmanuel Macron amesema mapema leo akiwa Beijing kwamba taifa hilo lina nafasi kubwa ya kufungua njia ya kupatikana kwa amani nchini Ukraine kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati yake na Urusi, ingawa ameonya kwamba Urusi haipaswi kupewa fursa ya kuwa na majadiliano ya kina na taifa hilo. Amesema hayo katika hotuba yake ya kwanza tangu alipowasili China kwa ajili ya ziara hiyo, alipokutana na raia wa Ufaransa, katika mji mkuu Beijing. Amesema Ufaransa inaweza pia kuwa sehemu ya jukumu hilo la kupatikana kwa amani na utulivu.

"Vita hivi ambavyo nimekuwa nikivieleza mara kwa mara kuwa ni vya kibeberu na kikoloni, vimekiuka misingi mingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Hivyo China, haswa kwa sababu ya uhusiano wake wa karibu na Urusi, ambao umethibitishwa tena katika siku za hivi karibuni, inaweza kuwa na jukumu kubwa," amesema Macron.

Kabla ya kuondoka Paris, Macron alizungumza na Joe Biden wa Marekani kuhusiana na ziara hiyo na msaada wao kwa Ukraine. Chanzo kimoja kimesema mazungumzo hayo yaliashiria nia ya pamoja ya mataifa hayo ya kuijumuisha China katika kuongeza kasi ya kumaliza vita na kurejesha amani ya kudumu. Jioni ya kesho Alhamisi anatarajiwa kukutana na viongozi wa China katika dhifa ya kitaifa.

Polen, Warschau | Staatsbesuch von Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr Zelenskiy na mkewe Olena Zelenska wakipokelewa na rais Andrzej Duda wa poland na mkewe Agata Kornhauser-Duda mjini Warsaw.Picha: Wojtek Radwanski/AFP/Getty Images

Zelenskiy azuru Warsaw.

Kutoka Beijing, Warsaw hii leo inakuwa mwenyeji wa rais Volodymyr Zelensky anayezuru taifa hilo jirani ambalo limepokea wakimbizi zaidi ya milioni moja kutoka Ukraine katika kipindi cha miezi 13 ya vita. Ziara yake inafanyika wakati Ukraine ikijiandaa kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika wiki ama miezi ijayo ili kuyatwaa upya maeneo ya mashariki na kusini kutoka kwa Urusi.

Zelenskiy atakutana na rais  Andrzej Duda na waziri mkuu Mateusz Morawiecki na atazungumza na wakimbizi na wananchi wa Poland pamoja na viongozi wa kibiashara ambao wanaweza kuhusishwa katika mchakato wa kuijenga upya Ukraine. Hii ni ziara ya tano ya nje ya Zelenskiy, tangu Urusi ilipowavamia February 2022, ikitanguliwa na ile ya Washington, London, Paris and Brussels.

Marekani yatangaza msaada mpya wa Ukraine.

Na huko Washington, taarifa zinasema Marekani imetangaza msaada mpya wa silaha kwa ajili ya Ukraine wa dola bilioni 2.6 na kufanya jumla ya msaada wake nchini humo hadi sasa kufikia dola bilioni 35.

Msaada huu mpya unatolewa wakati Ukraine ikijiandaa kuimarisha mashambulizi ya kushtukiza mashariki mwa nchi hiyo dhidi ya Urusi, ingawa bado haijweka wazi ni lini itaanzisha mashambulizi hayo.

Mapambano kwa sasa yanashuhudiwa zaidi katika mji uliozungukwa na madini na kitovu cha usafirishaji wa Bakhmut ulioko kwenye mkoa wa Donesk ambako eneo kubwa linadhibitiwa na Urusi. Pande zote zimepata hasara kubwa na mji huo kwa sasa umekuwa kama mahame kufuatia mapigano makali yaliyodumu kwa miaezi kadhaa.

Na taarifa kutoka Berlin zinasema kaimu kansela wa Ujerumani Robert Habeck kwa mara nyingine amelikumbusha taifa hilo kujua ukomo wake katika kuisaidia Ukraine, akionya halipaswi kuwa sehemu ya mzozo. Amesema hayo kabla ya kurejea nyumbani akitokea Kyiv alikokuwa kwa ziara ya siku mbili.