1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya vurugu Catalonia, watu 80 wajeruhiwa

John Juma
17 Oktoba 2019

Takriban watu 100 wakiwemo polisi 46 wamejeruhiwa katika jimbo la Catalonia kufuatia maandamano ya vurugu ambayo yamedumu kwa siku tatu mfululizo. Polisi zaidi kupelekwa jimbo hilo, huku maandamano zaidi yakitarajiwa.

https://p.dw.com/p/3RQmq
Katalonien Girona Quim Torra Protestmarsch
Picha: AFP/Generalita de Catalunya

Maafisa wa serikali nchini Uhispania wamesema watu 80, wakiwemo polisi 46 wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo, kufuatia maandamano makali yaliyogubikwa na vurugu na ambayo yamedumu kwa siku tatu zilizopita tangu hukumu ya kuwafunga jela wakuu wa harakati zilizoshindwa za jimbo la Catalonia kutaka kujitenga.

Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu wa mpito wa Uhispania imeeleza kuwa watu 33 wamekamatwa, na tayari waandamanaji wanne wamefungwa jela kwa mashtaka ya kusababisha vurugu.

Waandamanaji wameendelea na maandamano yao mapema leo, huku wakiweka vizuizi katika barabara za kaskazini mashariki mwa jimbo hilo, ikiwemo barabara kuu inayoelekea Ufaransa.

Kiongozi wa Uhispania Pedro Sanchez ameitisha mkutano na wataalamu kutoka wizara ya mambo ya ndani pamoja na wizara nyinginezo, kutathmini hali ya usalama kaskazini mashariki mwa jimbo hilo. Hapo awali Sanchez alisema:

"Serikali inasisitiza kuwa haitaruhusu vurugu badala ya utangamano. Ghasia, makundi ya vurugu au wale wanaotaka kuvunja sheria hawatafaulu. Ninataka kumsihi rais wa Catalonia Quim Torra na serikali yake. Wote wanajukumu la kisiasa na kimaadili kushutumu vurugu jimboni Catalonia bila ya kutoa visingizio."

Waandamanaji wakiweka vizuizi barabarani huku wakikabiliana na polisi mjini Barcelona.
Waandamanaji wakiweka vizuizi barabarani huku wakikabiliana na polisi mjini Barcelona.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Morenatti

Waziri wa ndani nchini Uhispania Fernando Grande-Marlaska amekiambia kituo cha televisheni cha Telecinco nchini humo kuwa serikali itapeleka maafisa zaidi wa polisi katika jimbo la Catalonia, ili kudumisha usalama.

Hapo jana, waandamanaji walichoma magari moto huku wakiwarushia polisi mabomu ya petroli, hali iliyozidisha vurugu kwenye maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu baada ya hukumu ya mahakama ya juu Uhispania, kuwafunga jela viongozi tisa wa juhudi za kutaka jimbo la Catalonia kuwa huru na lijitenge na Uhispania.

Kuhukumiwa kwa viongozi hao, akiwemo aliyekuwa makamu wa rais wa serikali ya jimbo hilo Oriol Junquares kumetonesha donda la uhusiano mbaya baina ya wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Catalonia na serikali kuu mjini Madrid.

Tangu Jumatano, maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana kuelekea makao makuu ya jimbo hilo, Barcelona, ambako wanafunzi pia wamekuwa wakiandamana huku vyama vya wafanyakazi vikitarajiwa kujiunga nao kesho kwa maandamano makubwa zaidi.

Maandamano zaidi ambayo yameitishwa na vyama vya wafanyakazi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa mjini Barcelona.
Maandamano zaidi ambayo yameitishwa na vyama vya wafanyakazi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa mjini Barcelona.Picha: AFP/Getty Images/P. Barrena

Kwa mujibu wa mashirika ya kutoa huduma za dharura, takriban watu 100 wamejeruhiwa kufuatia maandamano hayo ya vurugu.

Watu 58 walijeruhiwa mjini Barcelona akiwemo kijana mwenye umri wa miaka 17 aliyegonghwa na gari la polisi. Wengine 38 walijeruhiwa katika miji mingine ya jimbo hilo.

Hayo yakijiri, kiongozi wa Catalonia ambaye pia anaunga mkono jimbo hilo kujitenga Quim Torra, amesema lengo lake ni jimbo hilo kujitenga ifikapo mwisho wa mwaka 2021 ikiwa vyama vya jimbo hilo vitakubali.

Akihutubia bunge la jimbo hilo, ameongeza kuwa anataka pendekezo la kutaka kuwe na jamhuri ya Catalonia, liwe tayari ifikapo mwanzo wa msimu wa kuchipua mwaka ujao. Awali Torra alisema kutahitajika kura mpya ya maamuzi ya kutaka Catalonia kujitenga

Mnamo mwaka 2017, jimbo la Catalonia lilipiga kura ambayo haiukuidhinishwa na serikali kuu ya Uhispania ya kutaka kujitenga

Vyanzo: AFPE,RTRE,APE