1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yadhamiria kupanda idadi kubwa ya miti

Angela Mdungu
5 Juni 2020

Licha ya Ethiopia kutangazwa kuwa bado katika hali ya hatari kutokana na janga la virusi vya corona, Waziri Mkuu Abiy Ahmed bado amedhamiria kufikia lengo la mwaka huu la kupanda miti bilioni 5.

https://p.dw.com/p/3dJUy
Äthiopien - Weltrekord im Bäume pflanzen -Symbolbild
Picha: picture-alliance/G. Fischer

Mwaka uliopita, mamia ya wakulima walitumia siku moja kupanda miche 20,000 ya miti ya acacia nje kidogo ya mji wa Buee ulio karibu na mji mkuu, Addis Ababa nchini Ethiopia. Walikuwa wakiitikia wito uliotolewa mwezi Julai na Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye aliwataka wananchi wapande miti milioni 200 kwa siku na kuvunja rekodi ya dunia.
Lakini wakati wakulima wakiwa na matarajio makubwa wanasema kuwa, karibu mwaka mmoja baadaye wakati nchi hiyo ikielekea kuadhimisha siku ya mazingira duniani, matokeo ya miti iliyopandwa Buee yanakatisha tamaa.

Ewnatu Kornen, afisa wa mazingira wa eneo hilo anasema mvua zilizonyesha zilizoa zaidi ya theluthi ya miche iliyokuwa imepandwa na iliyobaki imekuwa ikiota kwa tabu kutokana na mashimo ambayo hayakuchimbwa inavyotakiwa yakiwa katika udongo usio na rutuba ya kutosha.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi nchini Ethiopia miche milioni 353 ambayo ni milioni 153 zaidi ya lengo la awali ilipandwa kote nchini humo wakati wa siku nzima ya kupanda miti mwaka jana. Hiyo ni sehemu ndogo tu ya miti bilioni nne iliyoripotiwa kupandwa katika msimu mzima wa mvua wa mwaka jana ambao huwa kati ya mwezi Juni hadi Septemba katika taifa hilo.

Äthiopien Addis Abeba | Premierminister Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: DW/Y. Gebregziabher

Upandaji wa miti mingi kwa mwaka huu bado haujapangwa, lakini Abiy ameitangaza siku ya Ijumaa kuwa mwanzo wa kampeni ya kupanda miti mipya bilioni tano itakayopandwa katika msimu wa mvua wa mwaka huu.


Nje ya Ethiopia, mjadala umekuwa umetawaliwa na ukweli juu ya idadi hii kubwa ya miche inayotajwa kupandwa.

Wataalamu watilia shaka uratibu wa upandaji miti  

Lakini wataalamu wa ndani wanasema yapo maswali muhimu ya kujiuliza: Je shughuli ya kupanda miti imeratibiwa vyema? Na je kuna ufuatiliaji wa kutosha ili miti hii iweze kukua?

"Si suala la idadi," anasema Negash Teklu, mkuu wa shirika lisilo la kiserikali linalohusika na Afya na mazingira liitwalo Population Health & Environment Ethiopia. Anasema "suala hapa ni kuhusu ufanisi wa mpango wa upandaji."
     
Mwezi uliopita, Abiy alitangaza kuwa asilimia 84 ya miti bilioni 4 iliyooteshwa mwaka uliopita imekua na kupongeza "juhudi kubwa za kuihudumia” zilizofanywa katika mwaka mzima wa 2019. Bado hakuna utafiti rasmi uliofanyika lakini Negash ambaye alisisitiza kuwa anaunga mkono ajenda ya upandaji miti ya wazirimkuu Abiy, inatiwa sana chumvi.

 "Hawakuangalia namna jamii inavyoweza kuimiliki hatua hii. Ilikuwa tu ni suala la-- 'Oh, tutapanda miti,'" Alisema Negash akizungumzia juhudi za mwaka jana.

 Hii ni katika mji mkuu Addis Ababa ambapo baadhi ya wakaazi walipanda miti ya mapambo katika msitu nje yam ji, wakati wengine wakiiweka miti mikubwa katika mitaa yenye shughuli nyingi ambako haina nafasi ya kuendelea kuwa na uhai.

Susan Edwards Gründerin des Institute for Sustainable Development Ethiopia
Susan Edwards, mwanzilishi wa taasisi ya Maendeleo Endelevu Ethiopia (ISD) akipanda miti shuleni.Picha: ISD

Ngesha anasema maafisa wanapaswa kufanya kazi maidi katika kupanda miche na pia kuwaeleza wananchi namna upandaji huo wa miti unavyoweza kuboresha maisha yao.

Wakati nchi hiyo ikiwa na matarajio ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu ambao bado haujapangwa ni lini hasa utafanyika, maafisa wanatarajia kuwa juhudi hizi  za kupanda miti zitasaidia kufuta mipaka ya tofauti za kikabila na mgawanyiko wa kisiasa na kuwaunganisha watu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa bustani ya Gullele ya mjini Addis Ababa Sileshi Degefa, wanataraji kuboresha Zaidi juhudi za kupanda miti mingi Zaidi itakayodumu. Anasema wamejifunza mengi kutoka katika shughuli hiyo ya upandaji miti ya mwaka uliopita na kwamba watapanda miche sahihi ya miti katika maeneo sahihi.

Chanzo: AFPE