1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Bunge labatilisha uchaguzi wa waziri mkuu

5 Mei 2014

Bunge la Libya limebatilisha kura iliyopigwa jana kumchagua waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, saa chache baada ya mtu aliyekuwa ametangazwa mshindi, Ahmed Maiteeq, kuapishwa kuchukuwa wadhifa huo.

https://p.dw.com/p/1Bto8
Uhasama wa kimakundi umelilemaza bunge la Libya
Uhasama wa kimakundi umelilemaza bunge la LibyaPicha: picture-alliance/dpa

Katika barua aliyoiandikia serikali na ambayo ilichapishwa katika tovuti ya serikali, Naibu Spika wa Bunge alitangaza kwamba mgombea huyo hakupata kura zinazohitajika. Uchaguzi huo wa jana Jumapili uligubikwa na hali ya vurugu, huku mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wabunge ukidhihirisha sura halisi ya msukosuko nchini Libya, ambako bunge na serikali imeshindwa kudhibiti hali ya mambo, huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa wanamgambo walioshiriki katika vita vya kumng'oa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Maafisa wakuu wa bunge walitoa taarifa zinazokinzana kuhusu matokeo ya uchaguzi wa waziri mkuu. Naibu wa kwanza wa spika Ezzedin al-Awami alisema kuwa licha ya kuongoza, mgombea Ahmed Maiteeq hakuwa amepata kura zinazohitajika.

Vuta nikuvute

Baadaye lakini ushindani wa madaraka uliibuka pale Naibu wa pili wa spika Saleh Makhzoun alipopinga yaliyosemwa na mkubwa wake, na kutangaza kuwa Maiteeq alikuwa amepata kura za kutosha, na hivyo kumtangaza rasmi kuwa waziri mkuu mpya, na kumtaka aunde serikali katika muda wa wiki mbili.

Abdullah al-Thinni, waziri mkuu aliyejiuzulu ambaye anaombwa kuendelea kuiongoza serikali
Abdullah al-Thinni, waziri mkuu aliyejiuzulu ambaye anaombwa kuendelea kuiongoza serikaliPicha: Reuters

Haikuishia hapo kwani Naibu wa kwanza Ezzedin al-Awami alirudi tena na kutangaza kuwa kura iliyopigwa ilikuwa batili, na hivyo kumuamuru Abdullah al-Thinni ambaye alijiuzulu wiki tatu zilizopita, kuendelea kuiongoza serikali.

Kufuatia tofauti hizo, maafisa hao wakuu wa bunge walibishana katika matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni, na kitakachofuata baadaye hakijulikani.

Wachambuzi wanasema iwapo Ahmed Maiteeq atathibitishwa kuwa waziri mkuu, atahangaika kupiga hatua yoyote kwa sababu serikali haina udhibiti juu ya wanamgambo walioshiriki katika vita vya kuuangusha utawala wa Kanali Muamar Gaddafi.

Uhasama wa kimakundi

Tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyouondoa madarakani utawala wa muda mrefu wa Kanali Gaddafi ambaye alijilimbikizia madaraka yote, mchakato wa demokrasia changa nchini Libya umekabiliwa na vizingiti, kutokana na uhasama wa kimakundi ndani ya bunge, na kuwepo kwa makundi yenye silaha ambayo yanakaidi mamlaka ya serikali.

Makundi ya wanamgambo wenye silaha yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa serikali mpya ya Libya
Makundi ya wanamgambo wenye silaha yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa serikali mpya ya LibyaPicha: Reuters

Waziri mkuu al-Thanni alijiuzulu wiki tatu zilizopita, akisema alikuwa akisema watu wenye silaha walikuwa wakitishia maisha ya familia yake.

Zoezi la kupiga kura kumchagua mrithi wake lilianza bungeni Jumatano iliyopita, lakini likaahirishwa baada ya wanamgambo wanaomuunga mkono mgombea aliyeshindwa kuvamia majengo ya bunge na kuwajeruhi watu kadhaa.

Bunge hilo lilikutana tena jana Jumapili, lakini likagubikwa tena na utata juu ya idadi ya kura alizopata Ahmed Maiteeg. Mbunge mmoja, Zainab Haroun al-Targi, ambaye aliwasilisha maoni ya wabunge wenzake wengi, alisema kura iliyopigwa kumchagua Maiteeq ilikuwa batili.

Bunge la Libya linazongwa na uhasama baina ya makundi yenye msimamo mkali wa kiislamu, yale yenye mrengo mkali wa kizalendo na mengine yenye mwelekeo wa kikabila.

Katika kile kinachoashiria matatizo mengine kwa nchi hiyo, makundi ya kikabila yamekiacha kituo muhimu cha mafuta cha El Sharara, lakini uchimbaji mafuta hauwezi kuanza tena hadi pale kundi jingine linalolidhibiti bomba la kusafirishia mafuta hayo litakapotoa ridhaa yake.

Upinzani wa makundi ya wanamgambo na ya kikabila umezorotesha uchimbaji wa mafuta ambayo ni chanzo muhimu cha mapato kwa Libya, na kuufanya mdogo kabisa ikilinganishwa na mwezi Julai ambapo mapipa milioni 1.4 yalikuwa yakichimbwa kila siku.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo