Vikosi vya Libya vyadhibiti meli ya mafuta | Matukio ya Afrika | DW | 11.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Vikosi vya Libya vyadhibiti meli ya mafuta

Serikali ya Libya imesema vikosi vyake vimeidhibiti meli ya mafuta yenye bendera ya Korea Kaskazini iliokuwa imetia nanga kwenye bandari inayoshikiliwa na wanamgambo wa mkoa ambako ilikuwa ikijaribu kupakia mafuta.

Meli ya mafuta yénye bendera ya Korea Kaskazini ikiwa imetia nanga bandari ya Al Sidra (08.03.2014)

Meli ya mafuta yénye bendera ya Korea Kaskazini ikiwa imetia nanga bandari ya Al Sidra (08.03.2014)

Mzozo huo uliotokea Al-Sidra mojawapo ya bandari kuu za kusafirisha nje mafuta nchini Libya umekuwa changamoto kubwa ka serikali kuu ya Libya. Bandari hiyo imekuwa ikishikiliwa kwa miezi kadhaa na wapiganaji wa mashariki ambao wamekuwa wakidai kupatiwa mamlaka zaidi ya kujitawala kutoka serikali ya Libya. Tukio hilo lenye kuihusisha meli ya mafuta ni jaribio la kwanza la kuuza mafuta kufanywa na watu wa mashariki ya Libya.

Adel al- Tarhouni wa Kundi la Operesheni ya Mapinduzi ya Libya ambalo ni kundi la wanamgambo lenye kuiunga mkono serikali amesema nahodha wa meli hiyo alisalimu amri wakati wa jioni hapo jana na kwamba meli hiyo ilikuwa imezingirwa kwa siku mbili na kundi la meli zenye wanamgambo wanaoiunga mkono serikali zikiwemo pia meli za uvuvi zenye mizinga na maroketi.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan amesema meli hiyo inahamishiwa kwenye bandari inayoshikiliwa na vikosi vya serikali.Amekaririwa akisema kwamba meli hiyo iko maili 20 kutoka magharibi ya Sidra na Ilikuwa ikichunguzwa kutoka angani na kwamba wameidhibiti kikimalilifu meli hiyo na wanaihaimishia kwenye mojawapo ya bandari zao.Ameongeza kusema watawakamata waliomo ndani ya meli hiyo na kuwafungulia mashtaka mahkamani.

Wahusika wa operesheni

Jeshi la Taifa la Libya.

Jeshi la Taifa la Libya.

Akizungumzia kadhia hiyo Waziri wa utamaduni wa Libya Habib al-Ameen amekanusha kwamba wanamgambo walihusika katika operesheni ya kuidhibiti meli hiyo na kusema kwamba ni vikosi vya taifa ndio yaani vya wanamaji ndio waliohusika katika operesheni hiyo. Pia amesema kwamba jaribio la kukaidi operesheni hiyo lilizimwa kwa matumizi ya nguvu lakini kulikuwa hakuna maafa yaliotokea.

Hata hivyo Essam al-Jahani ambaye anahusika na kundi la wanamgambo wa mashariki amekanusha madai hayo ya serikali kwamba inaidhibiti meli hiyo na amesema kundi lake limewakamata baadhi ya wapiganaji wanoiunga mkono serikali.

Kamanda wa wanamgambo wanaoshikilia bandari muhimu za kusafirisha nje mafuta mashariki ya Libya Ibrahim Jedran amesema katika taarifa leo hii kwamba wanaukaribisha msaada wa Marekani katika kufuatilia usimamizi wa usafirishaji nje wa mafuta na mapato katika mkoa wao wa mashariki.

Wanamgambo wakilinda bandari wanayoishikilia ya Al-Sidr.(08.03.2014).

Wanamgambo wakilinda bandari wanayoishikilia ya Al-Sidr.(08.03.2014).

Balozi wa Libya katika Umoja wa Mataifa Ibrahim Dabbashi ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mapipa ya mafuta 250,000 yalikuwa yamepakiwa kwenye meli hiyo ya mafuta yenye bendera ya Korea Kaskazini na kwamba fedha zilizolipwa kwa mafuta hayo zinatumiwa kwa hila na kundi hilo la wanamgambo lililopigwa marufuku.Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Libya meli hiyo inaaminika kuwa inamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa Ghuba.

Serikali ya Libya imeidhinisha operesheni ya kijeshi kurudisha udhibiti wa bandari tatu za kusafrisha nje mafuta zinazoshikiliwa na waasi wanaotaka kujitenga wanaodai kupatiwa fungu kubwa la mapato ya mafuta.Serikali kuu ya Libya imekuwa dhaifu tokea kupinduliwa kwa dikteta aliyetawala kwa muda mrefu nchini humo Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Yusuf Saumu