Lebanon yataka Saudi Arabia ifafanue kuhusu kujiuzulu kwa Hariri | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Lebanon yataka Saudi Arabia ifafanue kuhusu kujiuzulu kwa Hariri

Rais wa Lebanon Michel Aoun ameitaka Saudi Arabia kutoa ufafanuzi kwanini Waziri mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu akiwa Riyadh, Saad Hariri hajarejea nyumbani tangu kutangaza kujiuzulu kwake wiki iliyopita.

Mzozo wa kisiasa umeikumba Lebanon na kutikisa amani nchini humo tangu Hariri alipotangaza kujiuzulu mnamo tarehe 4 mwezi huu akiwa Saudi Arabia. Maafisa wa Lebanon wanasisitiza kuwa Hariri sharti arejee nyumbani huku kukiwa na uvumi kuwa anashikiliwa na Saudi Arabia.

Rais Auon ameitaka Saudi Arabia kueleza sababu zinazomzuia Hariri kurejea Lebanon. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amempigia simu Auon leo kujadili kujiuzulu huko kwa Hariri ambako hakukutarajiwa.

Rais wa Labanon amesema chochote kilichosemwa au kitakachosemwa na Waziri mkuu al Hariri  hakitachukulika kutoa taswira halisi kutokana na mazingira ya kutatanisha kuhusu hali yake isiyoeleweka nchini Saudi Arabia.

Saudi-Arabien Besuch Michel Aoun bei Salman bin Abulaziz Al-Saud in Riad

Rais wa Lebanon Michel Aoun na Mfalme wa Saudi Arabia Salman

Kujiuzulu kwa Hariri kwasababisha mtikiso

Auon amewaambia mabalozi wa nchi za kigeni kuwa al Hariri ametekwa nyara na lazima awe na kinga. Rais huyo amekuwa akifanya misururu ya mikutano ya ngazi ya juu na wanasiasa wa Lebanon na wanadiplomasia wa kigeni tangu al Hariri kujiuzulu ghafla.

Macron amesema nchi yake inaunga mkono umoja wa Lebanon na uhuru wake wa kujitawala. Marekani na Ufaransa zimeeleza kuiunga mkono nchi hiyo ili iweze kudumisha uthabiti wakati ambapo hali ni tete kati ya Lebanon na Saudi Arabia.

Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi amemtuma waziri wake wa mambo ya nje katika nchi za kiarabu kuhudhuria mazungumzo kuhusu mzozo wa kikanda uliosababishwa na kujiuzulu kwa Waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri.

Kujiuzulu huko kumeitumbukiza Lebanon katika mzozo na kusababisha uhasama kati ya nchi mbili mhasimu za Saudi Arabia na Iran. Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry atazizuru Jordan, Umoja wa falme za nchi za Kiarabu, Kuwait, Bahrain, Oman na Saudi Arabia kufanya mazungumzo ya pande mbili.

Shoukry pia atajadili kuhusu masuala yanayojiri katika kanda hiyo akiwa na ujumbe kutoka kwa Rais wa Misri al Sisi kuwa msimamo wa Misri ni kuona umoja wa nchi za Kiarabu unazingatiwa na pia kuepuka uhasama uanoweza kuathiri usalama wa kanda hiyo.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa/AFP/AP

Mhariri: Zainab Aziz