LEBANON ARAB LEAGUE | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

LEBANON ARAB LEAGUE

Nchini Lebanon mji wa Beirut unaripotiwa kuwa shwari japo wasiwasi umetanda huku Jeshi la Lebanon linaripotiwa kuendesha mapambano katika maeneo yaliyo nje ya mji wa Beirut.

default

Wapiganaji wa Hezbollah mjini Beirut


Wakati huohuo Jumuiya ya Milki za Kiarabu inajiandaa kutuma ujumbe maalum ili kutoa msukumo zaidi juhudi za upatanishi kati ya upinzani unaoongozwa na Hezbollah na serikali inayoungwa mkono na Marekani.Mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon ulianza mwezi Novemba mwaka jana baada ya Rais Emile Lahoud kumaliza muhula wake na mrithi wake kutopatikana mpaka sasa.


Majeshi ya serikali yaliingia katika maeneo ya milimani ya Druze kusini mashariki mwa mji mkuu wa Beirut.Mwishoni mwa wiki eneo hilo lilizongwa na mapigano makali kati ya majeshi ya serikali inayoungwa mkono na Marekani na wapiganaji wa upande wa upinzani wanaoongozwa na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.Mapigano makali yameendelea katika siku tatu zilizopita na kusababisha vifo vya yapata watu 40.


Hata hivyo hali inaripotiwa kuwa shwari hii leo mjini Beirut japo baadhi ya shule na majengo ya biashara bado yamefungwa kwa kuhofia mapambanao mapya.Ghasia hizo zilianza siku tano zilizopita.Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Milki za Kiarabu waliafikiana kupeleka ujumbe maalum wa upatanishi baada ya kufanya kikao cha dharura mjini Cairo nchini Misri hapo jana.Ujumbe huo utaongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Amr Moussa.Jumuiya hiyo kwanza ilitoa wito wa kusitishwa mapigano.Balozi Ahmed Bin Heli ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Milki za Kiarabu alisema kuwa ''kikao hiki kinatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na mashambulizi yote vilevile kujiondoa kwa wapiganaji waliojihami kwa silaha katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia.''


Azimio lililopitishwa na Jumuiya hiyo linatoa wito kwa wanasiasa wa Lebanon kuhudhuria mkutano utakaoshirikisha ujumbe wa wabunge ulio na dhamira ya kujadilia hali nchini Lebanon vilevile kupanga mikakati mbadala ya kudumisha amani.Mazungumzo hayo yanalenga kuwaleta pamoja Spika wa Bunge Nabih Berri,Kiongozi wa Kikristo Michel Aoun na kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah kwa upande mmoja na Waziri Mkuu Fouad Siniora,kiongozi wa chama kilicho na uwakilishi mkubwa bungeni Saad Hariri na rais wa zamani Amin Gemayel.


Duru za serikali zianaeleza kuwa majadiliano yanaendelea ili kuwezesha kikao maalum cha baraza la mawaziri kufanyika hii leo au kesho ili kuzungumzia hatua iliyochukuliwa na serikali hivi karibuni dhidi ya kundi la Hezbollah.Wiki jana serikali ya Lebanon iliamua kumfukuza kazi Kanali Wafik Choukair, mkuu wa idara ya usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Beirut vilevile kuchunguza mtandao wa mawasiliano ulioanzishwa na Hezbollah.Bwana Choukair ni mwandani wa kundi la Hezbollah.Uamuzi huo ulichochea mapigano hayo yaliyoanza wiki iliyopita.Hassan Nasrallah kiongozi wa Hezbollah

alisema kuwa ''Uamuzi huo ni sawa na kutangaza vita dhidi yetu.Suluhu yake ni kubatili maamuzi hayo yaliyofanywa na serikali ya Waleed Jumblatt ambayo si halali.La pili ni kumualika Nabih Berri kushiriki katika meza ya mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kitaifa.''


Mapambano hayo yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 40 yanaripotiwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 75 hadi 90.

Kundi la Hezbollah liliteka eneo kubwa la waislamu wengi lililo magharibi mwa mji mkuu wa Beirut na kudidimiza zaidi nchi ya Lebanon inayozongwa na mkwamo wa kisiasa.


Hata hivyo baadhi ya vizuizi vilivyowekwa na Hezbollah na wandani wao bado vipo barabarani nayo barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut bado imefungwa.Bunge nchini Lebanon linatarajiwa kukutana hapo kesho ikiwa ni mara ya 19 ya kujaribu kuteua rais mpya baada ya Emile Lahoud kumaliza muhula mwaka jana.Kwa sasa haijulikani iwapo kikao hicho kitafanyika. • Tarehe 12.05.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DyNl
 • Tarehe 12.05.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DyNl
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com