1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutunza 30% ya mazingira asilia duniani si jambo rahisi

15 Desemba 2022

Wawakilishi wa mataifa ya dunia waliokusanyika mjini Montreal kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai wanapigia upatu mkataba utakaotoa ahadi ya kuhifadhi asilimia 30 ya ardhi na bahari ifikapo mwaka 2030.

https://p.dw.com/p/4KxYJ
UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Themenbild
Picha: Christina Muschi/REUTERS

Tangu katikati kabisa mwa msitu ya Amazon hadi kwenye kina kirefu cha maji ya bahari ya Aktiki, kitisho ni dhahiri kwa makaazi ya viumbehai wa majini na nchikavu. Na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema ulimwengu unafaa kuhifadhi karibu theluthi ya eneo lake la ardhi na bahari ili kuokoa hatma ya mimea na spishi zinazoweza kutoweka.

Soma zaidi: COP15: Bioanuwai ni nini na kwa nini ni muhimu sana?

Wito huo ndiyo msingi wa majadiliano katika mkutano wa kilele wa Bayoanuai unaofanyika mjini Montreal nchini Canada. Iwapo maafikiano yatapatikana baada ya mkutano huo utakaomalizika wiki inayokuja, serikali duniani zitakuwa zimeweka ahadi ya kutenga asilimia 30 ya ardhi na maeneo yake ya bahari kama sehemu iliyohifadhiwa ifikapo mwaka 2030.

Hatua hiyo itaongeza maradufu eneo la ardhi iliyohifadhiwa duniani na mara tatu kwa maeneo ya bahari. Mataifa karibu 110 ikiwemo Marekani, Ufaransa na Canada yameonesha utayari wa kufikia lengo hilo.

Kipaumbele kwa tarakimu badala ya hali halisi

Lakini kama ilivyo kwa sera nyingine zote zinazotegemea sayansi, uchambuzi ni muhimu kufahamu iwapo lengo la kuhifadhi asilimia 30 ya eneo la dunia linaweza kweli kunusuru kutoweka kwa viumbehai na maakazi yake kwenye uso wa dunia.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Indigene Protestierende
Wakaazi asilia wa sehemu zinazotishiwa na mabadiliko ya tabianchi wakishinikiza wadau wa mazingira kuchukua hatua zinazofaaPicha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

"Hatari iliyopo, kama ilivyo kwa matukio yote yanayotawala na idadi kubwa ya wanasiasa, ni kwamba wao wanataka zaidi tarakimu" anasema Stuart Pimm, mtaalamu wa biolojia kutoka chuo kikuu cha Duke. Anasema wanasiasa wangetamani kuondoka kwenye mkutano wa Montreal na makubaliano ya kuhifadhi asilimia 30 ya sayari yetu, lakini kwa bahati mbaya lengo hilo halitoshi.

Soma zaidi: COP15: Bado hakujafikiwa mafanikio makubwa

Hadi sasa bado hakuna utafiti wa kutosha wa kisayansi unaounga mkono kuwa kuhifadhi asilimia 30 ya eneo la sayari ya dunia kutaondoa kitisho cha kuangamia kwa aina mbalimbali za viumbehai. Wataalamu wanasema hilo linategemea zaidi ubora wa uhifadhi kuliko ukubwa wa eneo linalohifadhiwa. Yaani kwa lugha rahisi, ulimwengu unaweza kunusuru kupotea kwa viumbehai kwa kuhifadhi kimkakati maeneo mahsusi kuliko kuweka lengo la kutenga asilimia 30 ya ardhi na bahari kuwa hifadhi.

"Kama tutafanya mambo yetu kwa werevu tutanusuru bayoanuai kwa kuyalinda maeneo yenye umuhimu mkubwa" anasema Pimm mtaalamu  wa biolojia.

Anasema kumekuwa na shauku ya kuyahifadhi maeneo ambayo kwa jumla hayana shughuli za watu na pia hayana maakazi makubwa ya viumbehai, mfano wa eneo lenye  theluji tupu huko Aktiki au jangwa la Sahara.

''Kuyalinda maeneo hayo siyo muhimu sana ikilinganishwa na kuhifadhi maeneo yenye idadi kubwa mimea na viumbehai vingine hata kama ni ngumu kufanya hivyo kutokana na idadi kubwa ya shughuli za binadamu,'' amesema mtaalamu huyo.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Antonio Guterres, UN-Generalsekretär
Katibu Mkuu wan Umoja wa Mataifa Antonio Guterres baada ya kuhudhuria ufunguzi wa mkutano huu wa Bayoanuai mjini MontrealPicha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

Utafiti mwingine wapendekeza hifadhi ya asilimia 44

Mtazamo wa mwana biolojia huyo unaungwa mkono na ripoti ya jarida la sayansi ililochapishwa mwezi juni mwaka huu ambayo ilionesha dunia inafaa kuhifadhi asilimia 44 ya ardhi yake ili kuzuia kupotea kwa viumbehai na kuharibika kwa ikolojia. Lakini changamoto iliyopo ni kuwa maeneo hayo ya ardhi yanayopendekezwa kuhifadhiwa ni nyumbani kwa watu karibu bilioni 1.8.

Maswali mengine yanayoundama mkutano wa Montreal ni iwapo lengo la kuhifadhi asilimia 30 lifanyika kwa ngazi ya dunia au nchi moja moja. Wataalamu na wawakilishi wanajenga hoja kuwa baadhi ya nchi duniani ni ndogo na hazina eneo kubwa la ardhi ya kutenga kwa uhifadhi huku nchi nyingine ni kubwa na zenye eneo kubwa la bayoanuai mfano wa Brazil na Indonesia zilizo na maeneo makubwa ya misitu.

Soma zaidi: Mkutano wa Bayoanuwai COP15 wafunguliwa Canada

Kuna suala pia la tafsiri ya neno uhifadhi. Wawakilishi wa mkutano Montreal ni lazima watoe majibu ya tafsiri ya neno hilo na kile kinachotarajiwa. Mathalan ni vipi nchi zitatekeleza uhifadhi? Je shughuli za binadamu kama uchimbaji madini au Maisha ya kawaida yanaweza kuendelea kwenye eneo lililohifadhiwa almuradi hakuna uharibifu wa mazingira unaotokea au maeneo yaliyohifadhi yazuiliwe kabisa kutumika kwa shughuli za watu?

Maswali yote hayo na mengine yatahitaji majibu kuelekea mwishoni mwa mkutano huo na hata baada ya wawakilishi wa mataifa duniani kukusanya virago na kuondoka mjini Montreal.

 

Chanzo: Reuters