1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Kutana na Siti binti Saad

25 Julai 2018

Siti Binti Saad kutoka kisiwa cha Unguja, Zanzibar, aliivunja miko ya Taarab na akawa mwanamke wa kwanza ambaye hajasoma kuimba mtindo huo wa muziki kwa Lugha ya Kiswahili.

https://p.dw.com/p/2xJPm

Siti binti Saad aliishi wakati gani? Siti binti Saad alizaliwa mnamo mwaka 1880 katika kijiji cha Fumba, Unguja ambacho ni kisiwa kikuu cha Zanziba ambayo kwa leo ni sehemu ya jamhururi ya Muungano wa Tanzania. Alizaliwa katika familia masikini. Aliuza udongo barabarani kabla ya kuhamia Zanzibar mjini mwaka 1911 kunapojulikana sasa kama Stone Town. Na hapo alianza kufanya kazi na wanamuziki, na akawa muimbaji maarufu wa muziki wa aina ya Taarabu. Aliendelea kuwa mwanamuziki wa Taarab hadi uzeeni. Alifariki mwaka 1950.

Siti binti Saad anajulikana kwa kipi? Siti binti Saad alikuwa ni nyota wa miondoko ya muziki wa taarabu, muziki ambao yeye mwenyewe aliupenda sana.  Alikuwa na sauti nzuri na ya kuvutia, alialikwa kutumbuiza katika nyumba ya sultani. Lakini Siti binti Saad hakuwaimbia tu wasomi, alitumbuiza pia mbele ya mihadhara ya watu wa kawaida na nyumba yake ilikuwa mahala pa kubadilishana mawazo na kufanyia mijadala.

Siti binti Saad
Picha: Comic Republic

Kipi kilimfanya Siti binti Saad kuwa miongoni mwa waasisi katika Taarab? Kabla yake, muziki wa taarabu ulikuwa unatumbuizwa na wanaume wasomi ambao mara nyingi waliimba kwa lugha ya kiarabu, lugha iliyokuwa ikitumiwa na wasomi wachache wa kisiwa cha Zanzibar. Siti binti Saad ambaye hakuwa na elimu rasmi alikuwa ni mwanamke wa kwanza aliepata umaarufu kwaajili ya uimbaji na aliupa umaarufu muziki wa taarabu kwa kuimba kwa lugha ya kiswahili. 
Kutokana na umaarufu wake, kampuni ya Gramophone ya Uingereza  ilimpeleka Bombay nchini India kuirekodi sauti yake, na kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kurekodi muziki na kutengeneza albamu kwa ajili ya mauzo.

Nyimbo za Siti bint Saad zinahusu nini? Nyimbo zake zinahusu maisha ya kila siku ya watu wa Zanzibar na zinazungumzia kuhusu matukio halisia. Zimebeba maudhui ya kuikosoa jamii, kupinga unyanyasaji wa matabaka, rushwa, unyanyasaji kwa wanaume na wanawake na mapungufu ya mfumo wa kisheria. Kwa namna hiyo, nyimbo za tarab zilizokuwa zikiimbwa na Siti binti Saadi zilikuwa ni siasa ya hali ya juu.

Kutana na Siti binti Saad

Nani alihamasishwa na Siti binti Saad? Siti binti Saad aliwahamasisha wanamuziki wengi na kufungua njia kwa waimbaji wa taarabu wanawake. Kwa mfano alikuwa ni mwalimu wa Bi Kidude, ambaye pia alikuja kuwa mwimbaji maarufu wa taarab. Siti binti Saad alikutana na mwandishi mashuhuri wa mashairi Shaaban Robert ambaye aliandika wasifu wake "Wasifu wa Siti binti Saad". Wasifu huo ulichapishwa mwaka 1956 baada ya kifo chake. Kitabu hiki ni kazi muhimu ya fasihi na kinatumiwa mashuleni. Shaabani Robert aliziita nyimbo za Siti binti Saad  kuwa ni fahari ya Africa Mashariki na kumbukumbu zake ni mwanga mkali gizani ulioachwa kwa vizazi vya siku za mbele. Chapisho la kwanza la 1988 la jarida la Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania linaloandika masuala ya wanawake lilimkumbuka Siti binti Saada kwa kuandika makala juu yake.

Urithi wa Siti binti Saad ni nini? Binti Saad alitunga na kuimba nyimbo zaidi ya 250, lakini nyimbo chache sana ndio zilizobaki hadi hii leo. Nyimbo zake zinachezwa sana Zanzibar, Tanzania na nje ya Tanzania. Nyimbo zake ni sehemu kubwa ya bendi nyingi za taarab. Mbali na hilo mwaka 2017, kulizinduliwa ufadhili wa mfuko wa Siti binti Saad, malengo yake ni kuhifadhi nyimbo zake na kukuza maadili na utamaduni wa Zanzibar.

Aude Gensbittle, Salma Said na Gwendolin Hilse  wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Mwandishi: Veronica Natalis

Mhariri: Iddi Ssessanga