Korti ya kijeshi kutoa uamuzi katika kesi ya Suu Kyi | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.04.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Korti ya kijeshi kutoa uamuzi katika kesi ya Suu Kyi

Mahakama ya kijeshi ya Myanmar itatoa uamuzi wa kesi ya ufisadi inayomkabili Aung San Suu Kyi siku ya Jumatano, katika kesi ambayo inaweza kumfanya mshindi huyo wa tuzo ya Nobel kufungwa jela miaka 15.

Suu Kyi, mwenye umri wa miaka 76, amezuiliwa tangu mapinduzi ya kijeshi yalipoiondoa serikali yake ya kiraia Februari mwaka jana, na hivyo kusitisha kipindi kifupi cha demokrasia nchini humo.

Tangu wakati huo amekumbwa na msururu wa mashtaka ya jinai, ikiwa ni pamoja na kukiuka sheria rasmi ya siri za taifa, rushwa na udanganyifu katika uchaguzi, na anakabiliwa na kifungo cha zaidi ya miaka 150 jela ikiwa atapatikana na hatia kwa makosa yote.

Uamuzi katika kesi ya ufisadi, ambapo Suu Kyi anatuhumiwa kupokea hongo ya dola 600,000 pesa taslimu pamoja na dhahabu, ilikuwa imepangwa Jumanne, kilisema chanzo kilicho karibu na kesi hiyo.

Lakini vikao "viliahirishwa" bila hukumu, ambayo sasa imepangwa Jumatano, chanzo hicho kiliongeza. Suu Kyi tayari amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa uchochezi dhidi ya jeshi, kukiuka sheria za Uviko-19 na kuvunja sheria ya mawasiliano ya simu, ingawa ataendelea kuwa chini ya kifungo cha nyumbani wakati akipambana na mashtaka mengine.

Waandishi wa habari wamezuiwa kuhudhuria vikao vya mahakama maalum katika mji mkuu wa kijeshi wa Naypyidaw na mawakili wa Suu Kyi wamepigwa marufuku kuzungumza na vyombo vya habari.

Suu Kyi anakabiliwa na jumla ya mashtaka 10 ya ufisadi, na kila moja ikiwa na uwezekano wa kifungo cha miaka 15 jela. Pia amefikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria rasmi ya siri za serikali, ambapo anashtakiwa pamoja na mwanachuoni wa Australia, Sean Turnell, ambaye pia amezuiliwa.

Kulingana na kundi la ufuatiliaji la eneo hilo, zaidi ya watu 1,700 wameuawa na zaidi ya 13,000 wametiwa mbaroni katika msako mkali dhidi ya wapinzani tangu mapinduzi hayo ya kijeshi.