1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini: Hatuna mpango wa mazungumzo na Marekani

Angela Mdungu
4 Julai 2020

Korea ya Kaskazini imesema haina mpango wa kuendelea na mazungumzo baina yake na Marekani hivi karibuni. Ni mazungumzo yanayoitaka kusitisha mpango wake wa nyuklia

https://p.dw.com/p/3emNP
Nordkorea Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Images/KCNA

 Mazungumzo hayo ni yale yanayolenga kuitaka Korea ya kaskazini iachane na mpango wake wa silaha za nyuklia. Akizungumza kupitia shirika la habari la taifa la Korea Kaskazini, naibu wa kwanza wa waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Choe Son Hui amesema leo 04.07.2020 kuwa, nchi yake haioni uhitaji wowote wa kukutana na Marekani.

Choe ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu minong'ono kuwa mkutano mwingine kati ya Raisi wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un, utafanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwezi Novemba mwaka huu.

Raisi wa Korea Kusini Moon Jae alipendekezwa tena kuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo. Kwa mujibu wa maafisa wake, wakati wa mkutano kwa njia ya video uliofanyika Jumanne iliyopita, Moon Jae alisema kuwa anataka kufanya kila liwezekanalo kuwakutanisha viongozi hao wa Marekani na Korea Kaskazini kabla ya uchaguzi wa Novemba.

Mshauri wa zamani wa Trump azungumza

Kwa upande wake, mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa kitaifa wa Marekani John Bolton, naye pia  alisema Trump atakutana na Kim, muda mfupi kabla ya uchaguzi iwapo tu anaamini kuwa hilo litasaidia katika harakati zake za kutaka kuchaguliwa tena kutetea kiti chake.

Vietnam Hanoi | Treffen Kim Jong-Un und Donald Trump
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alipokutana na Rais wa Marekani Donald Trump, Vietnam mwezi Februari, 2018Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Choe Son Hui amenukuliwa akisema "Marekani itakuwa imekosea sana kama inadhani mambo ya mazungumzo yatakuwa na mashiko kwetu".

Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo vikali vya kimataifa kutokana na mpango wake wa nyuklia. Mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini hayajaendelea tangu mkutano kati ya Trump na Kim nchini Vietnam mnamo mwezi Februari mwaka 2016.

Korea ya Kaskazini imesema mara kadhaa kuwa haina nia ya kuanza tena mazungumzo mapya hadi pale Marekani itakapoleta mapendekezo mapya.