1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia: Ufaransa na Ubelgiji zatinga nusu fainali

Sekione Kitojo
7 Julai 2018

Mapambano ya mwanzo ya  duru ya  robo fainali katika  kombe  la dunia  mwaka  huu 2018 nchini Urusi  yamemalizika, wakati  timu  za Ufaransa  na  Ubelgiji zimefanikiwa  kuingia  katika  duru  ya  nusu fainali.

https://p.dw.com/p/30z48
Fußball WM 2018 Brasilien - Belgien
Picha: Reuters/S. Perez

Ni mataifa matano tu ambayo  yamewahi  kushinda  kombe  la  dunia zaidi ya mara  moja. Hakuna  hata  moja  litakuwa  na  nafasi ya kushinda  taji  hilo  mwaka  huu. Mabingwa  mara  tano Brazil  na mabingwa  mara  mbili  Uruguay waliondolewa  katika  kinyang'anyiro cha  mwaka  huu cha  kombe  la  dunia jana Ijumaa katika  robo fainali. Argentina, taifa  jingine  lililofanikiwa  kutwaa  taji  hilo mara mbili , ilipokea  kipigo  katika  duru ya mtoano ya  timu  16 bora, wakati  mabingwa  mara nne  Ujerumani  waliayaaga mashindano haya  katika  awamu  ya  makundi.

Fußball WM 2018 Brasilien - Belgien
Wachezaji wa Brazil wakitoka uwanjani vichwa chini baada ya kufungwa na Ubelgiji Picha: Reuters/T. Hanai

Italia, ambayo  pia  ilishinda  mara  nne  taji  hili, hata  haikuweza kufuzu  kucheza  katika  fainali  hizi, ikipoteza nafasi  hiyo  kwa Sweden  katika  michezo  ya  mchujo.

Hii  ni  mara  ya  kwanza  kutakuwa  na   michuano  ya  nusu  fainali bila ya takriban Argentina, Brazil, Ujerumani  ama  Italia.

Kwa sasa  ni  Ufaransa  na  England pekee kama  mabingwa  wa zamani ambazo  bado  zina nafasi ya  kushinda  taji  hili  nchini Urusi.

Brazil  ilikuwa  moja  ya  timu  zilizopigiwa  upatu wakati  fainali  hizi zikianza nchini  Urusi, lakini Brazil  ilisumbuka mapema  katika awamu  ya  makundi  kuonesha  uwezo  wake na hatimaye  ilipoteza mchezo  wake  jana  dhidi  ya  Ubelgiji kwa  mabao 2-1 mjini Kazan.

Fußball WM 2018 Brasilien - Belgien
Nyota wa Brazil Neymar akiwa hana la kufanya ila kufuta machoziPicha: Reuters/T. Hanai

Baada ya  mwanzo wa kusua sua  katika  duru za  kufuzu kucheza katika  fainali  hizi, Brazil ilimuondoa  nahodha  aliyeshinda  kombe hilo  la  dunia  mwaka 1994 Carlos Dunga  na  kumteua  Tite  kuwa kocha  wa  ikosi  hicho.  Tite alileta  mabadiliko  haraka  katika matokeo ambayo  yalisababisha  Brazil  ufuzu  kucheza  katika fainali  hizi.

Licha  ya  kuwa  Brazil  ilimaliza  ikiwa  ya  kwanza  katika  kundi  E, ilishindwa  kukonga  nyoyo za  mashabiki katika  ushambuliaji. Kulikuwa  na vitu vya  hapa  na  pale kutoka  kwa  Neymar , ufundi na kasi  pamoja  na  Philippe Coutinho, lakini  timu haikuwa  ikicheza kwa uhuru kuelekea  golini kama wengi  walivyotarajia.

Fußball WM 2018 Brasilien - Belgien
Wachezaji wa Ubelgiji wakifurahia bao la pili dhidi ya Brazil Picha: Reuters/J. Sibley

Ngome ya Brazil

Kwa  kiasi  fulani  ngome  ya  Brazil  ilikuwa  imara , ikiruhusu  bao moja  tu  katika  awamu  ya  makundi hadi  katika  awamu  ya  timu 16 bora. Brazil  sasa imeondolewa na  mpinzani  kutoka  bara  la Ulaya  katika  awamu  ya  mtoano  katika  kila fainali nne  za  kombe la  dunia  tangu  ilipoweza  kutwaa  kombe  hilo mwaka  2002.

Uruguay  ilikuwa  mshindi  wa  kwanza  wa  kombe  la  dunia  mwaka 1930 na  nchi  hiyo  iliongeza  taji  la  pili miaka  20  baadaye  wakati ilipoishinda  Brazil  katika  mchezo  wa  fainali  mjini  Rio de Janeiro.

Fußball WM 2018 Uruguay - Frankreich
Mchezaji nyota wa Uruguay Luis Suarez akiwa na majonzi baada ya kuondolewa na Ufaransa katika robo fainali 2018Picha: Reuters/D. Staples

licha ya  kuwa Uruguay  haijafikia  katika  fainali  tangu  wakati  huo , wameweza kuwapo tena  katika  awamu  za  fainali.

Mwaka  2010 , Uruguay ilifika  katika  nusu  fainali , na  kupoteza dhidi  ya  Uholanzi  kwa  mabao 3-2. Timu  hiyo  ilifika  karibu  tena na  awamu  hiyo  mwaka  huu, lakini  ilishindwa  na  Ufaransa  jana kwa  mabao 2-0 mjini  Nizhny Novgorod.

Uruguay  ilikuwa ya  pili katika  kundi  la  mataifa  ya  Amerika kusini kufuzu  kucheza  katika  fainali  hizi  nyuma  ya  Brazil. Uwezo  wake mkubwa  iliyouonesha  nchini  Urusi  mara  hii, hususan  katika ushindi  wa  mabao 2-1 dhidi  ya  Ureno  katika  duru ya  timu 16, ilipandisha  matumaini  kwamba  timu  hiyo  inaweza  takriban kufikia uwezo  wake  wa  mwaka  2010.

Fußball WM 2018 Uruguay - Frankreich
Mwamuzi wa mchezo kati ya Ufaransa na Uruguay Nestor Pitana akizungumza na wachezaji wa Uruguay Suarez na Mbappe wa UfaransaPicha: Reuters/D. Sagolj

Hata  hivyo, wakati wa  kipigo  dhidi  ya  Ufaransa  katika  robo fainali, Uruguay  ililazimika  kucheza  bila  ya  mshambuliaji  wake aliyeumia Edinson Cavani. Na makosa  makubwa  aliyofanya  mlinda mlango Fernando Muslera  yalimzawadia Antoine Griezmann bao.

Leo michuano  ya  robo  fainali  ya  mwisho  inafanyika  wakati Sweden inatiana  kifuani  na  England  na  kisha wenyeji  Urusi wataingia  dimbani  kuoneshana  kazi  na  Croatia.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae

Mhariri: Idd Ssessanga