1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaunda kamati ya ushindi ya Odinga

Shisia Wasilwa
5 Juni 2024

Serikali nchini Kenya imeunda kamati maalum kumfanyia kampeni Raila Odinga anayewania uwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/4ggID
Kenya | Raila Odinga
Mgombea wa nafasi ya uwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Raila OdingaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwenye hotuba ya pamoja kwa wanahabari, Waziri Mwandamizi ambaye pia ni waziri wa masuala ya kigeni, Musalia Mudavadi, amesema kuwa Rais William Ruto angali anampigia debeRaila kupata kiti hicho.

Mudavadi amethibitisha kuwa kamati hiyo iliyoundwa inawajumisha washirika wa kisiasa wa Raila pamoja na maafisa wa serikali na lengo lake kubwa ni kusaidia mchakato wa kampeni.

Mipango ya kampeni ya kufanikisha ushindi wa Odinga


Mudavadi ameelezea kujitolea kwa serikali ya Kenya Kwanza kuona kuwa ndoto za Raila zinahuishwa "Kampeni zinaongozwa na serikali na maafisa wenye uzoefu na ufahamu. Idara ya masuala ya Wakenya walio nje ya taifa hilo imeanzisha sekreteriati ya kampeini inayojumuisha kikundi cha mikakati cha mgombea.” Alisema Mudavadi.

Kenia | Raila Odinga und in Nairobi
Raila Odinga wakati wa kutangaza kwa mgombea mwenza wake huko NairobiPicha: Raila Odinga press Team

Raila Odinga, ambaye alikuwa na uhasama mkubwa na William Ruto waliyewania pamoja urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita, amemmwagia sifa rais huyo wa Kenya kwa kuendelea kuwarai viongozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika kuunga mkono azma yake. Kwa Raila ushiriki wake sio tu kwa maslahi ya kisiasa nchini Kenya lakini, bara lote zima:

Odinga: Nina imani nitashinda

"Nimetiwa moyo sana na idadi ya maafisa wakuu serikalini waliojitolea, kuwa sehemu ya safari hii. Kwa kujitolea pamoja na ushirikiano huu mzuri kati yangu na serikali, nina Imani tutashinda kiti hiki.”
Aidha kiongozi huyo wa Azimio amewapongeza baadhi ya viongozi serikalini kwa kuunga mkono azma yake akisema maamuzi yao yamemshangaza. 

Kwa sasa, kamati hiyo ya kampeni inaanda maombi na nyaraka za Raila kwa lugha sita zinazotumika katika Umoja wa Afrika. Lugha hizo ni pamoja na Kifaransa, Kiingereza, Kiswahili, Kiarabu, Kireno na Kihispania kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Soma zaidi: Wakenya walia na bei mpya za petroli na dizeli

Hata hivyo, safari ya Raila ya kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika haitakuwa nyepesi kama inavyoonekena kwani mataifa ya Somalia na Djibouti pia yanawania kiti hicho. Mataifa 30 wanachama wa Jumuiya ya Kiislamu barani Afrika yametangaza kuiunga mkono Somalia.

Imesalia miezi miwili kabla ya kufungwa kwa mchakato wa kuwasilisha majina ya wagombea wanaokimezea mate kiti hicho katika Umoja wa Afrika.

DW Nairobi