1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKenya

Kenya inatafuta utulivu baada ya miaka 60 ya uhuru

12 Desemba 2023

Tangu Kenya ipate uhuru mnamo Desemba 12, 1963, nchi hiyo imekuwa na sehemu yake ya mapambano. Wakati majeraha ya unyanyasaji wa kikabila yanapona polepole, hali ya uchumi inazidi kuwa ngumu.

https://p.dw.com/p/4a3pq
Historia Kenya | Sanamu la mzalendo na mpigania uhuru Kenya Dedan Kimathi
Sanamu la kiongozi wa Kenya Dedan Kimathi ambalo limesimikwa katikati ya jiji la kiuchumi la Kenya NairobiPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Mwangaza uliojaa matumaini huku mkono wa kuume ukiwa juu ya bunduki yake: Sanamu la mpigania uhuru mashuhuri Dedan Kimathi  (pichani) ni rahisi kuonekana kwa mtu yeyote anaezuru jiji kuu la kibiashara la Nairobi.

Historia ya Kenya na mapambano yake ya uhuru kuanzia kutoka kwa mkoloni wa Uingereza zimehifadhiwa katika jiji la Nairobi. Sanamu la Kimathi limesimikwa katika barabara ya Jomo Kenyatta, ikipewa jina la mzalendo aliewaongoza Wakenya kudai uhuru na pia ndie aliekuwa rais wa kwanza wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Taifa hilo lilianza mwanzo mpya wakati mwanamfalme Philip ambae alikuwa ni mume wa Malkia Elizabeth II, alipokabidhi rasmi mamlaka mnamo Desemba 12,1963, na kutokea hapo "siku ya Jamhuri" ilianza kuadhimishwa.

Soma pia:Wakenya walia na bei mpya za petroli na dizeli

Miaka sitini baadae, si kila mmoja anafurahia matunda ya taifa hilo lililotazamwa kama mfano kwa mataifa ya Afrika mashariki. Berline Ndolo ni mwanzilishi na meneja wa programu katika shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu mjini Kisumu magharibi mwa Kenya la World Network for Sustainable Change, likisaidia kusukuma mbele ajenda ya elimu pamoja na kilimo anasema kupanda kwa gharama za maisha imesababisha Wakenya wengi kutoona umuhimu wa kusherehekea siku ya uhuru kama inavyojulikana "Jamhuri Day."

"Maisha yamekuwa magumu mno kwao, hawawezi kumudu hata milo mitatu kwa siku pengine hata miwili ya siku," Ndolo ameiambia DW na kuongeza kuwa kikubwa wanachokiangalia kwa sasa ni namna ya kuzimudu familia zao kwa mapato duni walionayo.

"Kupanda kwa gharama za maisha" ni msemo ambao umetawala nchini Kenya kwa sasa, huku Rais William Ruto ambae ametimiza mwaka mmoja madarakani akipunguza ruzuku na kuweka kodi mpya na kufanya hali kuwa mbaya zaidi miongoni mwa Wakenya.

"Rais alikuwa na ahadi kedekede na zenye matumaini makubwa kwa Wakenya" alisema Ndolo.

Hata hivyo kwa mtazamo wake anasema, kwa sasa hakuna kilichobadilika "biashara zinafungwa na wale ambao wameajiriwa wanatozwa ushuru mkubwa na hapo bado tunapambana kupata riziki." Aliiambia DW.

Kenya imeshinda mgawanyiko wa kikabila?

Historia ya Kenya ya hivi karibuni ilifafanuliwa na mapigano ya baada ya uchaguzi mnamo 2007 na mapema 2008.

Ushindi finyu lakini uliopingwa wa Mwai Kibaki, akitokea kabila la Kikuyu, dhidi ya Raila Odinga wa jamii ya Waluo, ulizua ghasia za kikabila zilizosababisha vifo vya zaidi ya 1,500.

Kenya | Wamasai wakiwa katika mkusanyiko wa kitamaduni
Wamasai kutoka Kenya wakiruka ikiwa ni moja ya ngoma ya kitamaduni.Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Peter Muchiri mwenye umri wa miaka 26 na ambae ni muhudumu wa hoteli katika mji uliopo katikati mwa Kenya wa Nyahururu anayataja machafuko hayo kama kengele ya hatari kwa taifa.

"Kwa kawaida kulikuwa na maeneo ulikuwa huwezi kwenda kuomba kazi au kutafuta msaada, ikiwa wewe si mtu kutoka eneo hilo, kwa sababu hakuna atakaekujali."

Muchiri ambae alikuwa na umri wa miaka 11 wakati mapigano yalipozuka katika mji wa Nyahururu uliotazamwa kama eneo salama kwa wakati huo.

"Taifa lilikuwa katika mkwamo mkubwa" alisema Muchiri na kuongeza kwamba "watu walijifunza kupitia ghasia hizo."

Kwa mtazamo wake anaona kwamba mgawanyiko wa kikabila umepungua kwa kiwango kikubwa tangu wakati huo, na sasa wengi wanazingatia utaifa badala ya ukabila.

Soma pia:Kenya yatikiswa na wimbi jipya la maandamano ya upinzani

Kwa upande wake James Shikwati ambae ni mwanzilishi wa taasisi ya  Inter Region Economic Network anasema rais Ruto amekuwa na mafanikio fulani katika dhana ya kuumaliza ukabila nchini humo.

"Amefanikiwa kuifanya Kenya isitegemee kwenye kabila fulani, na kuondoa ile kabila hili, kabila lile" Shikwati alisema.

Urais wa Ruto haukosolewi kwa dhana ya kikabila

Kulingana na Shikwati, hii pia ilimaanisha mabadiliko makubwa katika jinsi Wakenya sasa wanavyoutazama utawala wa Ruto.

"Wakenya wanatathmini uongozi wake kwa nadharia pana," lakini si kwa mtazamo wa kikabila.

Kenya | Rais Willium Ruto akiwa na Mfalme wa Uingereza Charles III
Rais wa Kenya Willium Ruto akiteta jambo na Mfalme wa Uingereza Charles III wakati wa ziara ya Mfalme Charles III Kenya mnamo mwezi Oktoba mwaka huu.Picha: Arthur Edwards/The Sun/empics/picture alliance

"Hawamtaji kwa jina la kabila lake," alisema. "Wanaangazia uchumi tu. Wanasema haufanyi vizuri, watu wanapoteza kazi, makampuni yanafungwa."

Sera za Ruto ziliposababisha bei kupanda, Wakenya wengi waliingia mitaani. Maandamano hayo makubwa na wakati mwingine yenye vurugu yalichochewa naRaila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya ambaye alikataa kukubali kushindwa kwake baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa 2022. Maandamano hayo yamekoma, lakini ugumu wa kiuchumi bado ungali unawasakama Wakenya.

Samir Hassan ni baba wa watoto wanne na dereva huko Mombasa pwani ya Kenya, jiji la pili kwa ukubwa nchini Kenya. Ratiba yake mara kwa mara inampeleka kwenye kingo za magharibi mwa jiji ambapo Reli ya kisasa ya SGR inaunganisha pwani ya Kenya na mji mkuu Nairobi.

Soma pia:Rais Ruto awaomba wapinzani Kenya kutoa nafasi kwa mazungumzo

Treni hiyo iliyojengwa na China inawapeleka watalii mara tatu kwa siku, lakini kutokana na wengi kukabiliwa na matatizo ya kiuchumi, watalii hao hawafiki tena.

"Sasa kila Mkenya anapunguza gharama," Hassan aliiambia DW.

"Kwa kawaida, tuna shughuli nyingi sana mwezi wa Desemba kwa sababu ni mahali ambapo watu wanapumzika na ndipo tunapata wateja mchanganyiko, wageni na watalii wetu wa ndani.

Matatizo ya kiuchumi na mustakabali wa Kenya

Msururu wa mikopo na mlima wa madeni unaokua kwa kasi kulingana na Shikwati, na upendeleo katika mfumo wa fedha wa kimataifa na maamuzi potofu ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa pia ulitekeleza wajibu wao.

Lakini maamuzi ya Ruto kama rais, ikiwemo kusitisha ruzuku na kuanzisha kodi mpya, hakika hayakuwa mwarobaini wa mzozo wa kifedha.

Polisi Kenya yazuia maandamano ya upinzani

"Uchumi wetu ni kama vile sisi Kenya tunawaita wachuuzi - watu wanaobeba vitu na kuuza barabarani. Kwa hivyo uchumi wa aina hii unanunua bidhaa China na kuwauzia Wakenya si afya." Alifafanua Shikwati.

Kwa mantiki hiyo kutoza kodi kubwa kwa uchumi ambao hauna tija, kufunga makampuni na kusababisha mzigo mkubwa kwa watu wa kawaida kunaliacha taabani taifa hilo.

Soma pia:Serikali ya Kenya kudhibiti mfumuko wa bei

Miaka sitini baada ya uhuru ubaguzi wa kikabila si hoja ya msingi miongoni mwa Wakenya kwa wakati huu. Isipokuwa ni matatizo ya kiuchumi ambayo yanatishia mustakabali wa taifa hilo ambalo lilipigiwa mfano kwa mataifa jirani.