1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kisiasa Kenya unazidi kupanuka kuelekea uchaguzi

25 Oktoba 2017

Kenyatta, anayetarajiwa kushinda kipindi cha mwisho katika uchaguzi wa siku ya Alhamisi nchini Kenya, ni mtoto wa rais wa Kwanza wa taifa hilo hayati Jomo Kenyatta, mtu anayeangaliwa kama mmoja wa wasomi wa taifa hilo

https://p.dw.com/p/2mVE3
Kenia nach der Annulierung der Präsidentenwahl | Uhuru Kenyatta
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kenyatta aliye na miaka 55 tajiri na aliyekamilisha masomo yake nchini Marekani, ambaye familia yake inamiliki ardhi na biashara kadhaa nchini Kenya amefuata mfano wa babake wakati alipomshinda mpinzani wake Raila Odinga na kuwa rais wa kenya mwaka 2013.

Kenyatta alishinda tena katika uchaguzi uliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu kwa asimilia 54 ya kura lakini Mahakama ya juu ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi huo kufuatia madai ya udanganyifu na kuamuru uchaguzi mpya. Rais Kenyatta alikubali uamuzi wa Mahakam lakini kwa hasira huku akiwaita majaji hao "wakora" huku akitishia kufanya mabadiliko katika mahakama hiyo pindi atakaposhinda uchaguzi siku ya Alhamisi ambayo pia ni siku yake ya kuzaliwa.

Kwa upande wake kiongozi wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga amesema hatoshiriki katika uchaguzi mpya akidai hautakuwa wa huru na haki. Kufuatia matamshi yake na kujiondoa katika kinyanganyiro cha urais Kenyatta sasa analazimika kuchuana na wagombea wadogo wadogo ambao wengine katika uchaguzi uliyopita walipata chini ya asilimia moja ya kura zilizopigwa. Kenyatta hata hivyo alianza tena kampeni zake kwa fujo, akizuru maeneo tofauti ya Kenya huku akimkejeli mpinzani wake pamoja na mahakama  ya juu.

Kenia Raila Odinga bei Kundgebung in Mombasa
Picha: Reuters/J. Okanga

 "Tuko tayari kwa uchaguzi hata kama atashiriki au," alisema rais Kenyatta wakati mpinzani wake Raila Odinga alipojitoa katika kinyanganyiro hicho huku akitania kuwa hakuna mahala popote katika katiba palipoandikwa ni lazima Raila Amollo Odinga awepo katika zoezi la uchaguzi.  Hatamu ya kwanza yauongozi ya rais Kenyatta imeelezewa kutumia fedha nyingi kuimarisha miundo mbinu n ahata ukuaji wa uchumi, lakni hii imekwenda sambamba na ongezeko la madeni na kutokuwepo na usawa. Ugaidi pia limekuwa tishio kubwa huku Kenyatta akilazimika kulihutubia taifa baada ya mashambulio mabaya mwka 2013 na 2015.

 Kenyata ameshika nafasi kadhaa za uongozi kabla ya kuwa Rais

Kenyatta aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na hata Naibu Waziri Mkuu alizaliwa mwaka 1961 muda mfupi baada ya babake Jomo Kenyatta kutolewa korokoroni baada ya kushikiliwa kwa takriban muongo mmoja. Na kabla ya kuwa rais wa kwanza wa Kenya mwaka 1964.

Jina lake la kwanza  la Rais huyo, ni neno la kiswahili, linalomaanisha  Uhuru. Alisoma shule binafsi mjini Nairobi ya St Marys kisha akaendelea na masomo yake katika chuo cha Amherst nchini Marekani na kusomea sayansi ya siasa na uchumi. Kenyatta anaonekana kama kiongozi katika kabila la wakikuyu miongoni mwa makabila makubwa nchini Kenya. Ameoa na amebarikiwa na watoto watatu na mara kwa mara anahudhuria kanisa la kikatoliki.

Kenia Päsident Kenyatta
Picha: Reuters/B. Ratner

Aliingia kwa mara ya kwanza katika siasa baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama tawala wakati huo cha  KANU kilichokuwa kikiongozwa na babake. Baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho wakati wa serikali ya Daniel Arap Moi . Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2002 alihudumu kama kiongozi wa upinzani bungeni kwa muda mchache baadaye akamuunga mkono Rais Mwai Kibaki katika uchaguzi wa urais mwaka 2007 na kuchaguliwa kama Waziri Mkuu na pia Waziri wa Fedha wakati serikali ya Mwai Kibaki ilipoundwa.

Aliwahi kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC  kupanga machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008 na kushtakiwa kwa uhalifu dhidi ya binaadamu. Baadaye aliunda chama chake cha TNA kisha akateuliwa mgombea urais kupitia chama hicho na kushinda uchaguzi wa mwaka 2013 hatua iliyompa nafasi ya kuwa rais wa nne wa taifa la Kenya:

Mwandishi Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman