1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yapiga marufuku samaki kutoka China

Josephat Charo
17 Oktoba 2018

Wafanyabiashara wa samaki wanashusha pumzi baada ya marufuku ya kuagiza samaki kutoka nje ya nchi ya Kenya mahsusi China kutangazwa. Rais Uhuru Kenyatta ametangaza marufuku hiyo Jumatano (17.10.2018)

https://p.dw.com/p/36iMK
Kenia Frank Osean, fish seller from Kayole, Kenya
Frank Osien, mchuuzi wa samaki katika kitongoji cha Kayole jijini Nairobi, KenyaPicha: DW/T. Mwadzaya

Tangazo hilo la kupiga marufuku uagizaji samaki kutokea nchi za kigeni limetolewa baada ya wafanyabiashara wa sekta hiyo kulalamika kuhusu ushindani mkubwa sokoni. Akiwa kwenye kikao cha kujadili masuala ya wafanyabiashara wadogo katika chuo kikuu cha biashara cha Strathmore, Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa ipo haja ya kuwa na ujanja kwenye biashara.

Mwezi wa Juni mwaka huu wavuvi kutokea eneo la ziwa Naivasha walilalamika kuwa samaki wa kigeni wamejaa sokoni jambo linalowasakama koo wafanyabishara wa humu nchini.Itakumbukwa kuwa mwaka 2016 gavana wa zamani wa kaunti ya Kisumu Jack Ranguma aliirai serikali kuu kuweka marufuku kamili ya kuagiza samaki kutokea nchi ya China kwani hilo linakwamisha biashara.

Kwa upande wa pili, idara ya ubora wa bidhaa nchini Kenya ina mtazamo tofauti. Tathmini ya mwaka 2018 ya Idara inayosimamia ubora wa bidhaa nchini Kenya, Kenya National Bureau Of Standards, inatahadharisha kuwa wakenya watasubiri muda mrefu zaidi kabla ya kuona tofauti kwani samaki wanaovuliwa nchini hawatoshi.

Samaki wamepungua

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya samaki imekuwa ikipungua kwa muda wa miaka mitatu mfululizo kutokea tani alfu 98 mwaka 2016 hadi tani alfu 92 mwaka uliopita kutoka Ziwa Viktoria. Hilo limesababishwa na magugu maji yaliyoenea na mbinu zisofaa za uvuvi kadhalika idadi ya samaki aina ya Sangara kupungua.

Kenia Fried Tilapia fish
Samaki aina ya Sangara katika soko moja mtaa wa Kayole, NairobiPicha: DW/T. Mwadzaya

Samuel Owino Dera, mwanaharakati wa eneo la Dunga Beach kaunti ya Kisumu, alisisitiza kuwa wanajitahidi kuyalinda mazingira wanakozaa samaki kwenye Ziwa Viktoria.

Hali ni yiyo hiyo katika Ziwa Turkana ambako idadi ya samaki waliovuliwa wamepungua kutokea tani alfu 70 mwaka 2016 hadi alfu 4 mwaka uliopita.Chanzo cha hali hiyo ni mbinu zisofaa za uvuvi na kuhifadhi samaki pamoja na maji ya Ziwa Turkana kukauka.

Hali sio tofauti katika uvuvi wa samaki wa bahari ya Hindi kwani idadi ya samaki na viumbe vyengine vinavyoliwa imepungua kwa 3.7% kutokea tani alfu 24 mwaka 2016 hadi alfu 23 kwa sasa. Kamba na pweza kwa pamoja hawakutimiza 10% ya viumbe vinavyovuliwa kutoka baharini. Changare John ni mkazi wa Gazi katika kaunti ya Kwale na analalamika kuwa kamba wamepotea kwa muda.

Samaki wanaofugwa nao pia wamepungua sokoni kwasababu ya ongezeko la bei ya chakula na mabadiliko ya hali ya hewa yanayofanya vidimbwi kukauka.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW Nairobi

Mhariri: Josephat Charo