1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Vifo kufuatia uunganishaji wa umeme kwa njia haramu

Wakio Mbogho28 Aprili 2021

Watu 93 wamepoteza maisha kutokana na uunganishaji haramu wa umeme nchini Kenya katika kipindi cha miezi 10.

https://p.dw.com/p/3sglL
Eco Africa Sendung
Picha: DW

Wakenya wengi wanalalamikia gharama ya juu ya maisha pamoja na kunyanyaswa na kampuni ya umeme nchini humo, licha ya mpango wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme kuonekana kuzaa matunda. 

Kampuni ya umeme ya Kenya imetoa tahadhari kwa umma kuhusu uunganishaji wa umeme kinyume cha sheria wanaosema unaendelezwa sehemu nyingi nchini na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.

Soma pia:Taa za jua zapunguza makali ya umaskini Kenya

Akizungumza mjini Nakuru, Meneja msimamizi wa maswala ya usalama wa kampuni hiyo John Oguda ameeleza kuwa kati ya mwezi Julai mwaka jana na Aprili mwaka huu, watu 93 wamepoteza maisha yao baada ya kurushwa na umeme.

"Tumekuwa na matukio mengi ya uunganishaji haramu wa umeme. Watu wengine pia wanawatumia makanjanja kuwawekea nyaya za umeme. Watu hawafahamu hatari iliyo mbele yao ndiposa kama kampuni tumeamua kuuhamasisha umma,” amesema Oguda.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa kufikia sasa wameweza kuwafikia Wakenya milioni 34.1 kutoka idadi ya awali ya milioni 12.8.
Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa kufikia sasa wameweza kuwafikia Wakenya milioni 34.1 kutoka idadi ya awali ya milioni 12.8.Picha: Baz Ratner/REUTERS

Mradi wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme

Mwaka 2017 serikali ya Kenya kupitia kampuni ya umeme, ilianzisha mradi wa kuwaunganisha Wakenya wote na umeme uliopewa jina "Last Mile Connectivity”, lengo likiwa kuhakikisha kuwa taasisi zote muhimu kama vile shule na hospitali zimepata umeme.

Soma pia: Kenya, bila nishati hakuna maendeleo

Wakenya walioko maeneo yenye miundo mbinu hafifu kama vile vijijini na maeneo ya mabanda pia ni walengwa kwenye mradi huu. Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa kufikia sasa wameweza kuwafikia Wakenya milioni 34.1 kutoka idadi ya awali ya milioni 12.8.

"Mitaa yetu imekuwa salama kutokana na mradi huu, na wafanyabiashara wanaendeleza kazi zao hata usiku bila uoga. Tunapoendelea kuwaunganisha watu zaidi na umeme tunajenga uchumi wa saa 24 nchini mwetu. Zaidi ya miaka 50 baada ya uhuru wengi wetu waliishi bila umeme kwa sababu ya mipangilio mibovu na dhana potovu,” alisema Rais Kenyatta.

Kenya imewekeza pia kwenye mradi wa kuzalisha umeme kutumia upepo.
Kenya imewekeza pia kwenye mradi wa kuzalisha umeme kutumia upepo.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Malalamiko ya ada za juu ya kampuni ya umeme Kenya

Licha ya mafanikio haya Wakenya wamezidi kulalamikia ugumu wa maisha, mara kwa mara kampuni ya umeme ya Kenya ikijikuta inalaumiwa kwa kuwanyanyasa wananchi.

Kwenye mitandao ya kijamii pia, kampuni ya umeme ya Kenya imelaumiwa kwa kutoza ada za juu kupindukia, huduma zisizo madhubuti na uzembe.

Wengine wameelezea kukwera na ukosefu wa ushindani kwenye huduma ya umeme na hata kutishia kugeukia matumizi ya nguvu za nishati ya jua.

Hata hivyo, kampuni ya umeme ya Kenya inaushauri umma kupata mwongozo kutoka kwao ili kuepukana na ajali zaidi.