Kenya kutuma wanajeshi DRC kupambana na ugaidi | Matukio ya Afrika | DW | 22.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya kutuma wanajeshi DRC kupambana na ugaidi

Wanajeshi wa Kenya wanatarajiwa kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulisaidia jeshi la Kongo katika kupambana na ugaidi na pia kufanikisha kumaliza vurugu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Rais wa Kongo Félix Tshisekedi ametangaza hayo mjini Kinshasa akiwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anayezuru Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mbali na masuala ya ulinzi na usalama, nchi hizo mbili pia zimetia saini mikataba mingine kadhaa. 

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya walitia saini hapo jana Jumatano mbele ya marais wao, mkataba wa ushirikiano wa jumla pamoja na mikataba mingine maalum.

Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi

Matumaini ya marais Tshisekedi na Kenyatta ni kwamba mikataba hiyo, itaimarisha uhusiano wa urafiki na ushirikiano kwa ajili ya maendeleo na kuwafaidi raia wa pande zote mbili.

Rais Kenyatta na mwenyeji wake Felix Tshisekedi pamoja na wajumbe wao wakati wa ziara ya kitaifa ya Kenyatta mjini Kinshasa Aprili 21, 2021.

Rais Kenyatta na mwenyeji wake Felix Tshisekedi pamoja na wajumbe wao wakati wa ziara ya kitaifa ya Kenyatta mjini Kinshasa Aprili 21, 2021.


Kuhusu ulinzi na usalama, Tshisekedi alitangaza kwamba hivi karibuni, kutakuwepo hatua kali za kijeshi dhidi ya magaidi katika eneo la mashariki mwa Kongo, kutokana na ushirikiano kati ya wanajeshi wa Kongo na Kenya.

"Katika wiki zijazo, wanajeshi wa Kenya watawasili Kongo kusaidia vikosi vyetu, ili kutatua kwa njia bora zaidi shida hii ya ugaidi na vurugu mashariki mwa nchi yetu. Nawaomba kila mtu awe tayari kwani mashambulio yetu hayatakuwa na huruma hadi kukomesha kabisa vurugu huko Mashariki," amesema Tshisekedi.

Vijana wa DRC waandamana dhidi ya MONUSCO

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya zimesaini pia makubaliano katika nyanja za kidiplomasia na kiuchumi.

Baadhi ya wanajeshi wa Kenya wanaopambana na wanamgambo wa Alshabaab nchini Somalia. (Picha ya maktaba)

Baadhi ya wanajeshi wa Kenya wanaopambana na wanamgambo wa Alshabaab nchini Somalia. (Picha ya maktaba)

Na hivyo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza kufunguliwa ofisi za ubalozi mdogo katika miji miwili hapa nchini.

"Ili kuendeleza uhusiano mzuri kati ya nchi zetu mbili, Kenya imejitolea kuanzisha ofisi za ubalozi mdogo huko Goma na pia ubalozi wa heshima huko Lubumbashi ili kuendelea kukuza uhusiano kati ya nchi zetu mbili," amesema Rais Kenyatta.

Leo Alhamisi rais Kenyatta anamaliza ziara yake hapa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Uhusiano kati ya nchi hizi mbili umeimarika sana. Tukumbuke kwamba Kenyatta ndiye rais pekee aliyehudhuria hafla ya kuapishwa Felix Tshisekedi kama rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.