1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kalonzo ajiunga tena na kikosi cha Azimio One Kenya

2 Juni 2022

Joto la siasa limepanda Kenya zikiwa zimesalia siku 66 kabla ya uchaguzi mkuu. Kikosi cha Azimio La Umoja One Kenya kimepata mshirika mpya, Kalonzo Musyoka aliyerejea baada ya kukosa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza

https://p.dw.com/p/4CCwi
Kenia Wahl Politiker Raila Odinga (L) und  Kalonzo Musyoka
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Wakati huohuo, William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza anaurai Umoja wa Ulaya kuwa chonjo kwa madai kuwa inaandaliwa njama ya kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao. Wakati hayo yakiarifiwa, tume ya uchaguzi IEBC imekamilisha zoezi la kuhakiki maelezo ya wapiga kura ikisubiri kuhitimisha shughuli ya kuhakiki hati za wagombea wa nyadhfa mbalimbali.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amefungua ukurasa mpya baada ya kurejea kwenye muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na kuridhia kutwaa nafasi ya waziri kiongozi aliyoahidiwa. Kalonzo Musyoka aliyasema hayo kwenye kikao na waandishi wa habari mtaani Karen jijini Nairobi.

Soma pia: Kenya kupata makamu wa Rais wa kwanza mwanamke?

Kwa mantiki hii, ameifutilia mbali azma yake ya kuwania urais. Kiongozi huyo wa Wiper Demokratik pia aliahidi kumuunga mkono na kumpongeza Martha Karua kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga anayeipeperusha bendera ya Azimio la Umoja One Kenya.

Kenia | Raila Odinga und in Nairobi
Raila alimteuwa Karua kuwa mgombea mwenzaPicha: Raila Odinga press Team

Wakiwa mtaani Langata jijini Nairobi Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karuawalinadi sera zao kwa umma. Raila Odinga aliwahakikishiwa wakaazi wa Nairobi kuwa Azimio ndio dawa ya Kenya.

Wakati huo huo, naibu wa Rais William Ruto amedai kuwa majina kiasi ya milioni ambao ni wafuasi kwenye ngome zake waliosajiliwa yamefutwa kwenye daftari la wapiga kura.

Akizungumza na wajumbe wa Umoja wa Ulaya, William Ruto aliweka bayana kuwa majina hayo yamefutwa kwa njia isiyoeleweka na kuwarai waingilie kati kuokoa mchakato wa uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake, tume ya uchaguzi na mipaka IEBC inajiandaa kukagua na kutathmini kwa kina maombi ya watu milioni 1 ya kutaka kuhamishiwa vituo vya kupigia kura.

Tetesi zimezagaa kuwa majina hayo yalibadilishiwa vituo pasina ridhaa ya waliosajiliwa kupiga kura. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, IEBC Wafula Chebukati anakiri kuwa baadhi ya walioomba kuhamishiwa vituo vya kupigia kura hawakuwa na hati za uthibitisho ila daftari litakaguliwa.

Daftari hilo la wapiga kura linafanyiwa tathmini baada ya ukaguzi wa wapiga kura kukamilika na litachapishwa rasmi wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu na kutangazwa kwenye vituo vya kupigia kura.

William Ruto wa Kenya Kwanza na Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya wanaowania urais watawasilisha hati zao tarehe 4 na 5 mtawalia mwezi huu kwa tume ya IEBC.

Thelma Mwadzaya DW Nairobi.