1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kupata makamu wa Rais wa kwanza mwanamke?

16 Mei 2022

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, mwanamke ameteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais. Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amemteua Martha Karua wa chama cha NARC-Kenya kuwa mgombea mwenza wake.

https://p.dw.com/p/4BNIZ
Kenia | Raila Odinga und in Nairobi
Picha: Raila Odinga press Team

Wakati huohuo, kiongozi wa Wiper Democratik Kalonzo Musyoka amejiondoa kwenye muungano wa Azimio la Umoja-OKA na kutangaza atawania urais kivyake.

Kwenye uwanja wa jumba la mikutano la kimataifa KICC uliosheheni wafuasi na wanasiasa, mgombea wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja-OKA Raila Odinga alimtaja Martha Karua kuwa mgombea wake mwenza.

Alikuwa kwenye orodha ya mwisho ya watatu bora

Kwa upande wake, Martha Karua ambaye ni mwanasiasa aliye na uzoefu wa miaka mingi aliahidi kuitumikia Kenya na kuwa watawajibika.

Kenia | Raila Odinga und in Nairobi
Charity Ngilu (kushoto) Martha Karua (katikati) na Raila Odinga (kulia)Picha: Raila Odinga press Team

Martha Karua wa chama cha NARC-Kenya aliibuka mshindi baadaya kuwa kwenye orodha ya watatu bora waliokuwa wanawania nafasi ya ugombea wenza. Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo wa NARC-Kenya aliwahi kuwa mbunge wa Gichugu kwa zaidi ya miaka 20 na waziri wa maji na sheria katika vipindi tofauti. Aliwahi pia kuwania urais mwaka 2013 na ugavana wa kaunti ya Kirinyaga mwaka 2017. Wazazi wake wamemsifu kwa ujasiri wake. Jackson Karua ni baba mzazi wa Martha Karua.

Mamake mzazi Josephine Wanjiru Karua ameelezea kuwa mwanawe alikuwa na uwezo wa kuongoza tangu utotoni.

Kalonzo Musyoka ajitenga na muungano wa Azimio

Kwa upande mwengine,uteuzi huo umezua hisia mseto ndanina nje ya muungano wa Azimio la Umoja-OKA. Kiongozi wa Wiper Demokratik iliyokua kwenye muungano huo,Kalonzo Musyoka amejiondoa na kutangaza kuwania urais kivyake.

Kalonzo Musyoka Kenia Vize Präsident
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo MusyokaPicha: AP Photo

Duru zinaeleza kuwa tayari amewasilisha jina lake kwa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC ili aweze kuwania urais.

Wakati huohuo, kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi anadai kuwa muungano wa Azimio la Umoja-OKA hauna msingi thabiti na utasambaratika.

Aliyaeleza hayo mtandaoni kwenye ukurasa wake wa Facebook.Kampeni rasmi za uchaguzi mkuu zimepangwa kuanza tarehe 29 mwezi huu wa Mei.