Kagame akutana na Macron | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kagame akutana na Macron

Rais Paul Kagame wa Rwanda leo amekuwa na mazungumzo mjini Paris na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, katika jitihada  za kufungua  ukurasa mpya katika Uhusiano wa nchi hizo mbili, uliozorota  kwa karibu miaka 24

Kuzorota huko kulitokana hatua ya dola hilo kubwa kuwaunga mkono waliofanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994.  Mohammed Abdul-Rahman anawasimulia zaidi juu ya ziara hiyo. Ni mara ya kwanza  kwa rais Paul Kagame wa Rwanda kukutana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Ikulu ya Elyseee mjini Paris tokea  2011, wakati ambapo uhusiano wa nchi hizo mbili  bado haujaimarika, ikiwa ni miaka 24 tokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda  1994.

Rais kagame ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa Umoja wa Afrika, yuko mjini Paris  ambapo kesho Alhamisi atahudhuria ukumbi wa kimataifa wa kiufundi  unaojulikana kama VivaTECH. Kabla  ya hafla hiyo watakula  chakula cha  pamoja  cha jioni na wakuu wa makampuni ya kiufundi  wakiwemo Mkuu wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg na Satya Nadella kutoka kampuni ya Microsoft. Rwanda inawania kuwa  kituo kikuu cha masuala ya ufundi barani Afrika.

Kagame na Macron walishakutana  mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja, kwanza wakati wa mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini NewYork na baadae nchini India katika mkutano kuhusu matumizi ya nishati ya Jua mjini New Delhi. Pia  Macron anapanga kuhudhuria mkutano wa kilele wa  Umoja wa Afrika , kama mgeni mualikwa, mkutano utakaofanyika Mauritania mwezi Julai.

Frankreich Präsident Emmanuel Macron & Paul Kagame, Präsident Ruanda (Reuters/C. Platiau)

Picha ya pamoja ya rais Kagame na mwenyeji wake Macron

Wamekubaliana pamoja na utata uliopo

Baada ya mazungumzo yao katika Ikulu ya Elysee, Macron na Kagame walitoa taarifa ya pamoja, ambapo walizungumzia azma yao ya kutaka kushirikiana  licha  utata ulioyagubika mahusiano ya nchi zao mbili. Taarifa hiyo ilitaja pia juu ya kubadilishana mawazo katika nyanja  kadhaa kama  vile uvumbuzi,  masuala ya tabianchi  na harakati za kusimamia amani barani Afrika.

sambamba na hayo  Kagame na Macron walitarajiwa kugusia uwezekano wa  Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Luoise Mushikiwabo kuwa mgombea wa wadhifa wa Katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa- Francophonie,  ambayo kwa sasa inaongozwa na  Michaelle Jean  Mcanada mwenye asili ya Haiti.

Jitihada za kumaliza tofauti kati ya Rwanda na Ufaransa

Miaka 24 baada ya mauaji ya Kimbari, Rwanda na Ufaransa bado zimo katika jitihada ya kurekebisha uhusiano wao.Ufaransa ilikiri makosa kuhusiana na mauaji hayo, lakini  imeyakataa madai ya Rwanda kwamba ilikula njama katika mauaji hayo kwa kuliunga mkono jeshi la Wahutu waliohusika na sehemu kubwa ya mauaji . Zaidi ya Watutsi na wahutu wa msimamo wa wastani 800,000 waliuwawa. Akikumbusha   kilichotokea  wakati wa mahojiano hapo mapema  na  kituo kimoja cha matangazo  cha Ufaransa TV 5 Monde ;waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo alisema " Ufaransa kupitia maafisa fulani wakifaransa waliowaunga mkono waliokuwa kwenye utawala uliofanya mauaji ya  kimbari Rwanda tangu miaka  23 iliopita, wanajaribu kufunika kuhusika kwao. Hiyo ndiyo historia ya  Ufaransa na Rwanda tangu 1994."

Mnamo mwaka 2010  aliyekuwa rais wa Ufaransa  wakati huo Nicolas Sarkozy  alikiri  kwamba Ufaransa ilifanya makosa makubwa, lakini hakuomba radhi. mnamo mwaka 2015, rais wa zamani Francois Hollande aliahidi kuruhusu kuwekwa wazi kumbukumbu zote za Ufaransa kuhusiana na mauaji ya  kimbari nchini Rwanda 1994, pamoja na Operesheni ya kijeshi ya Ufaransa . Wakati Kagame ambaye  wakati huo alikuwa kiongozi wa  kundi la wapiganaji wa RPF na kutwaa madaraka siku chache baadae, amewatuhumu maafisa wa Ufaransa kwa kuunga mkono utawala wa Wahutu uliokuwa madarakani, Ufaransa ilidai jeshi lake lilijiingiza kati sio tu kuwaokoa raia wake waliokuweko nchini humo, bali pia  kuzuwia mauaji.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com