1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson atishia kuachana na mpango wa Brexit

Daniel Gakuba
22 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza ametishia kuachana na makubaliano ya Brexit aliyofikia na Umoja wa Ulaya na kuelekeza nguvu katika maandalizi ya uchaguzi mpya, ikiwa bunge mjini London litapiga kura kuyakataa makubaliano hayo.

https://p.dw.com/p/3RjB4
UK London Boris Johnson
Picha: picture-alliance/PA Wire/V. Jones

Boris Johnson haonekani kulegeza kamba katika mvutano baina ya serikali yake na wabunge wanaompinga, ambao wamepania kuyazuia makubaliano yaliyofikiwa baina ya serikali ya Johnson na Umoja wa Ulaya kuhusu uhusiano wa baadaye baina ya Uingereza na umoja wa huo, baada ya mchakato wa Brexit kuhitimishwa.

Akizungumza mwanzoni mwa mjadala wa bungeni siku ya Jumanne, Johnson amewataka wabunge kuyaunga mkono makubaliano yake, ili kumaliza mkwamo uliopo na kusonga mbele.

''Kama bunge hili litayaridhia makubaliano haya, ambayo naamini ni mema kwa maslahi ya Uingereza na kwa Umoja wa Ulaya, tutaachana na maandalizi ya dharura kwa uwezekano wa kuondoka bila makubaliano, na badala yake tuelekeze nguvu katika kujenga uhusiano wa baadaye na majirani zetu wa Ulaya,'' alisema Johnson.

England Brexit Parlamentssprecher John Bercow
Bunge likiendelea na mjadala kuhusu Brexit.Picha: picture-alliance/empics/House of Commons

Kitisho cha kuyaondoa makubaliano

Lakini pamoja na rai hiyo kwa wabunge, Waziri Mkuu Johnson pia ametoa onyo, akisema ikiwa bunge litaamua kurefusha muda wa mchakato wa Brexit hadi Januari au zaidi, atayaondoa makubaliano hayo, na kujikita katika kuandaa uchaguzi mpya.

Johnson ambaye alichukua wadhifa wa waziri mkuu mwezi Julai, kwa ahadi ya kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 kwa hali yoyote ile, amewaambia wabunge kuwa kamwe hatoruhusu mchakato huo kuendelea kwa miezi mingine.

Jioni ya Jumanne wabunge wanapiga kura mbili; ya kwanza wakiulizwa kimsingi kuyakubali au kuyakataa makubaliano na Umoja wa Ulaya, na ya pili kuhusu ratiba inayopendekezwa na serikali kuyajadili makubaliano hayo na pengine kuyafanyia marekebisho.

Hata hivyo, chama cha upinzani cha Labour kimesema kitaridhia uchaguzi mpya, ikiwa tu Uingereza itaafikiana na Umoja wa Ulaya kurefusha mchakato wa Brexit kwa muda wa kutosha kuandaa uchaguzi wa mapema, na kuhakikisha kuwa hakuna uwezekano wa Uingereza kuondoka kiholela katika umoja huo.

Großbritannien Brexit
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uingereza, Jeremy Corbyn.Picha: picture-alliance/dpa/PA Wire/D. Lawson

Juncker: Brexit homa kubwa

Kizungumkuti cha Brexit kimejitokeza pia katika bunge la Ulaya mjini Strasbourg Jumanne, katika kikao cha kutathmini muhula wa rais wa halmashauri ya Ulaya anayemaliza muda wake Jean Claude Juncker. Juncker amesema Brexit imekuwa homa kubwa katika kipindi chake ofisini.

''Kusema kweli imeniumiza sana, kutumia muda wangu mwingi ofisini nikishughulikia Brexit, badala ya kuangazia masuala ya kuimarisha muungano wetu na kuboresha maisha ya watu wake. Brexit imekuwa kupoteza muda na nguvu.''

Zinabakia siku tisa tu kisheria, hadi kumalizika kwa muda wa uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Chanzo: Mashirika