Johnson ahoji malipo ya wakurugenzi wa Thomas Cook | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Johnson ahoji malipo ya wakurugenzi wa Thomas Cook

Bada ya kampuni ya Utalii ya Thomas Cook kufilisika, Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amehoji sababu ya viongozi wa Kampuni hiyo kujilipa fedha nyingi wakati kampuni hiyo ilikuwa ikielekea kufilisika

Akizungumza akiwa mjini New York, Johnson amehoji ni kwanini serikali iwajibike kutokana na matendo ya wakurugenzi waliokuwa wakilipwa mishahara minono. Johnson amesema Kampuni hiyo ya utalii ilipaswa kuwa na bima kwa ajili ya hali kama iliyoikumba.

Kampuni ya Thomas Cook imefilisika baada ya deni lake kufikia dola bilioni 2.1 lililotokana na mikataba mibovu iliyotokana na uhasimu wa biashara mtandaoni. Kampuni hiyo ililazimika kunadi takribani safari milioni tatu za mapumziko kwa mwaka ili kurejesha riba.

Tangazo la kufilisika kwa kampuni hiyo lilitolewa mapema Jumatatu baada ya kushindwa kufanya makubaliano na udhamini wa serikali ama  wanaoidai kampuni ya Thomas Cook.

Kuidhamini Thomas Cook ilikuwa sawa na kupoteza fedha

Serikali ya Uingereza kupitia waziri wa biashara Andrea Leadsom imesema hakukuwa na maana ya kuidhamini kampuni hiyo kwani kufanya hivyo kungekuwa sawa na kupoteza fedha za walipa kodi kwenye biashara ambayo haikuwa ikikidhi mahitaji ya wateja wake.

Thomas Cook Passagiere am Flughafen Palma de Mallorca

Abiria katika uwanja wa ndege wa Mallorca, baada ya kampuni ya usafiri na utalii ya Thomas Cook kufilisika

Hii ilisababisha hali ya taharuki katika hoteli ambazo baadhi ya wateja wa Thomas Cook wamekuwa wakitakiwa kulipa bili zao na hali kampuni hiyo ikiwa haina fedha.

Kwa mujibu wa mdhibiti wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya udhibiti wa anga wa Uingereza,Richard Moriarty ndege za dharura ziliwarejesha watu 14,000 nchini Uingereza siku ya Jumatatu na wengine zaidi ya 135,000 wanatarajiwa kurejea ndani ya siku 13.

Katika hatua nyingine, ndege zote za shirika la Condor la Ujerumani ambazo ni kampuni tanzu ya Thomas Cook iliyofilisika  zinaendelea na shughuli zake kama ilivyopangwa. Kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo, timu maalumu zimepelekwa katika viwanja mbalimbali vya ndege ili kujibu maswali yoyote ambayo wasafiri wanataka kuuliza.