1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Faini zitalipwa na nahodha, wahudumu na wamiliki wa chombo

12 Juni 2019

Serikali ya Italia imetoa kanuni ya kuanza kuwatoza faini watu na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayowaokoa wakimbizi baharini na kuwafikisha katika bandari za Italia bila ya idhini

https://p.dw.com/p/3KE9V
Lampedusa Sea Watch Flüchtlinge dürfen an Land
Picha: Reuters/N. Jaussi/Sea-Watch

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yatakayopatikana na hatia ya kuwaokoa wahamiaji na kuwaleta bandarini yatalazimika kulipa faini ya kati ya dola elfu kumi na moja hadi dola elfu hamsini na sita, vile vile vyombo vya baharini ambavyo vitaendelea kufanya shughuli hizo hata baada ya kutozwa faini vitakamatwa na kufungiwa daima. Faini hizo zitalipwa na nahodha, wahudumu wa chombo na wamiliki wake.

Kanuni hiyo pia inawaruhusu maafisa wa polisi kuchunguza visa vya ulanguzi wa watu kwa njia za siri, na inarahisisha kufuatiliwa kisiri kwa mawasiliano ya watu wanaoshukiwa kufanya ulanguzi wa binadamu. Zaidi, waziri wa usalama wa ndani Matteo Salvini atakuwa na nguvu ya kuyaamuru mashirika ya uokozi kulipa faini hizo, jukumu ambalo lilikuwa ni la wizara ya uchukuzi na miundombinu.

Mittelmeer Rettung von Flüchtlingen durch Sea-Watch 3
Wahamiaji wakiwa ndani ya chombo kuingia ItaliaPicha: picture-alliance/ROPI/SeaWatch/N. Jaussi

Kanuni hiyo imekawia kutekelezwa baada ya kupata pingamizi kutoka kwa Umoja wa Mataifa na ofisi ya rais wa Italia Sergio Mattarella. Katika kikao cha baraza la mawaziri hapo Jumanne waziri Salvini aliisifu kanuni hiyo kwa kusema ni hatua wamepiga katika usalama wa taifa na ana uhakika inaambatana na sheria zote za ndani na kimataifa.

Salvini amekaza kamba kwa wahamiaji

Serikali ya Italia inaundwa na vyama vya siasa kali vya mrengo wa kushoto maarufu Vuguvugu la Nyota Tano na mrengo wa kulia maarufu Liga. Waziri Salvini ambaye pia ni kiongozi wa Liga amekuwa akiongoza kubuniwa kwa kanuni mbali mbali za kukabiliana na wahamiaji tangu alipoteuliwa kuwa waziri wa usalama wa ndani mwaka mmoja uliopita, ikiwemo kanuni ya Disemba mwaka jana ya kuondoa usaidizi wa kiutu kwa wahamiaji ambao hawastahiki kupewa hifadhi kama wakimbizi.

Tangu mwaka 2014, zaidi ya watu laki sita wamevuka bahari ya Mediterenia kufika nchini Italia wakikimbia vita na ufukara barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati. Katika safari hiyo ya hatari, zaidi ya wakimbizi elfu kumi na nne wamekufa maji ama hawajulikani waliko. Kwa sababu ya kukosa vibali vya kuingia Ulaya, wamekuwa wakiwalipa walanguzi wa watu ili kuwavusha kupitia mashua zisizokuwa madhubuti.

Seenotrettung Schiff Iuventa
Polisi wakiwa pambizoni mwa mashua ya shirika lisilokuwa la kiserikali Picha: Getty Images/B. Francesco

Kwa sababu kazi ya kuwatafuta na kuwaokoa wakimbizi ilisitishwa, jukumu la kuwasaidia wakimbizi hao wanaojaribu kuvuka bahari limewaangukiwa wahudumu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Tangu mwaka 2014, mashirika hayo yamekuwa yakiingiza kiasi cha wakimbizi elfu 30 kwa mwaka nchini Italia.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mtaifa linaloshughulikia Wakimbizi, UNHCR, na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, zinaeleza kwamba tangu mwanzo wa mwaka huu kiasi cha watu 1,940 wameingia Italia kutoka Kazkazini mwa Afrika na 350 wamefaiki wakiwa safarini, idadi inayoweka kiwango cha waliofariki kuwa zaidi ya asilimia 15. Idadi ya wahamiaji imepungua katika miaka ya hivi karibuni ila mji mkuu wa Italia, Rome, bado unakabiliwa na wakimbizi wanaoingia kinyume cha seria. Hadi mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, maombi ya waliotaka kupewa hifadhi ya kuwa wakimbizi ilikuwa zaidi ya watu laki moja na elfu thelathini na tano.

(DW)