1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israeli yamsaka muuaji wa wanajeshi wake

Admin.WagnerD14 Desemba 2018

Vikosi vya Israel vinaendelea kumsaka mpalestina anaetuhumiwa kuwauwa wanajeshi wawili wa Israel katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

https://p.dw.com/p/3A8Up
Syrisch- israelische Grenze - Syrische Armee
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Msako huo unaendelea wakati ambapo waziri mkuu Benjaminn Netanyahu anashinikizwa  na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia apitishe hatua kali kujibu kitendo hicho. 

Shambulio la jana Alkhamisi lilikuwa baya kabisa kuwahi kufanywa na wapalestina waliokuwa na silaha katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan tangu miezi miwili iliyopita, na kuzusha maandamano ya makundi ya walowezi dhidi ya Netanyahu ambae serikali yake ya mrengo wa kulia inategemea uungaji mkono wa jamii hizo za walowezi.

Vyombo vya habari vya Israel vinaashiria uwezekano wa kuzuka wimbi jipya la malalamiko ya wapalestina-Intifada dhidi ya Israel kudhibiti ukingo wa magharibi.

Katika shambulio la jana, mtu aliyekuwa na bunduki alitoka ndani ya gari na kuwafyetulia risasi wanajeshi na watu wengineo nje ya makaazi ya wayahudi katika eneo la kati la ukingo wa magharibi. Amewauwa wanajeshi wawili  na kuwajeruhi  wengine wawili vibaya sana kabla ya kutoroka.

Msako mkali mjini Ramallah 

Westjordanland Razzia in Jenin nach Mord an Rabbi Raziel Shevack
Picha: picture-alliance/Zuma Press/M. Turabi

Jeshi la israel limeuzingira mji wa Ramallah yanakokutikana makao makuu ya kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na kutoa wito wa kuzidishwa idadi ya wanajeshi.

Mapigano kati ya wapalastina na wanajeshi wa israel yameripuka katika maeneo mengine ya ukingo wa magharibi ikiwa ni pamoja na eneo la kati ya Ramallah jeshi sa Israel lilipoanza hujuma zake.

Walowezi wa kiyahudi wakihanikiza kwa makelele na kuyavurumishia mawe magari ya wapalestina huku mwarabu ambae ni dereva wa basi akipigwa na yahudi mmoja wa itikadi kali katika eneo la Modiin.

Israeli yawatia nguvuni wapalestina kadhaa

Israelischer Premier Benjamin Netanjahu
Picha: AFP/Getty Images/J. Hollander

Jeshi la Israel limewakamata wapalestina 40 wengi wao wanasemekana kuwa na mafungamano na wafuasai wa itikadi kali wa Hamas waliodai kuhusika na mashambulio mawili ya hivi karibuni. Hamas hawakusema kama wanahusika na shambulio la jana lakini maafisa wa Israel wanawatuhumu.

Kuna hofu ya kuripuka maandamano  ya wapalastina baada ya sala ya ijumaa leo.

Wakati huo huo vikosi vya ulinzi vya wapalastina vimepambana na wafuasi wa Hamas katika mji wa Hebrone na miji mengine ya ukingo wa magharibi. Maandamano yameitishwa kuadhimisha siku ya kuasisiwa kundi la wafuasi wa itikadi kali wa Hamas.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/

Mhariri: Mohammed Khelef