1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yadai kuwashikilia wanamgambo 500 wa Kipalestina

22 Machi 2024

Jeshi la Israel limeendeleza operesheni katika hospitali ya Al-Shifa na kusema inawashikilia mamia ya wanamgambo. Hayo yanajiri wakati juhudi zikiendelea za kutaka kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano Gaza.

https://p.dw.com/p/4e0UA
Tel-Aviv I Daniel Hagari, Msemaji wa Jeshi la Israel
Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagari akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Wizara ya Ulinzi mjini Tel-Aviv: 18.10.2023Picha: Gil Cohen-Magen/AFP

Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagari amesema kuendelea kwa operesheni ya kijeshi iliyoanza siku ya Jumatatu katika hospitali kubwa ya Gaza ya al-Shifa, kumewawezesha kuwakamata wanamgambo zaidi ya 500 wa Kipalestina ikiwa ni pamoja na mamia ya wapiganaji wa  Hamas na wale wa kundi la Islamic Jihad.

Maafisa wa usalama na makamanda wa kijeshi  ni miongoni mwa waliokamatwa. Hagari amesema vikosi maalum vya jeshi la Israel vimetumia " mbinu ya udanganyifu" na kuwavamia wapiganaji hao, huku akisisitiza kuwa wameyadhohofisha mno makundi hayo:

" Magaidi wengi katika hospitali ya al Shifa, na hasa magaidi wa Islamic Jihad, walijisalimisha kwa wanajeshi wetu. Hili ni pigo kubwa mno kwa kundi la Islamic Jihad. Wengi wa wanamgambo wao wa kaskazini wamejisalimisha au kuuawa katika operesheni hiyo hadi sasa."

Gaza  | Wapalestina wakiondoka al-shifa kutokana na mashambulizi ya Israel
Wakaazi wa Ukanda wa Gaza wakiwemo watoto wakiondoka na vitu vyao vichache katika hospitali ya al-shifa kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel eneo hilo.Picha: Dawoud Abo Alkas/Anadolu Agency/picture alliance

Israel ilitangaza pia hapo jana kuwauwa wanamgambo 140 wa kundi la Hamas katika hospitali hiyo, taarifa iliyokanushwa na kundi la Hamas kwa kusema kuwa Israel imekuwa ikidanganya mara kadhaa na kusababisha maafa makubwa kwa raia.

Juhudi za kufikiwa mpango wa usitishwaji mapigano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewasili hii leo mjini Tel-Aviv ambapo anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kujadili kuhusu mzozo huu wa Gaza.

Soma pia: Mashambulizi ya Israel katika hospitali ya al-Shifa yaua watu 140

Mbali na mpango wa usitishwaji mapigano, Blinken atazungumza na Netanyahu kuhusu suala la usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo la Palestina na kuitaka Israel kutoanzisha operesheni yake ya ardhini katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, ambako ni kimbilio la karibu watu milioni 1.5.

Tel-Aviv I Antony Blinken akiwasili nchini  Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwasili mjini Tel-Aviv nchini Israel kukutana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu mzozo wa Gaza.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapiga kura leo Ijumaa juu ya azimio lililopendekezwa na Marekani ambalo linaelezea ulazima wa kusitisha mara moja mapigano katika vita vya Israel na Hamas. China imesema hii leo kuwa inaunga mkono hatua za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kusitisha mapigano huko Gaza, lakini Beijing ambayo ni mjumbe wa kudumu wa baraza hilo aliye na kura ya turufu, haikuweka wazi ikiwa itaunga mkono rasimu ya azimio la Marekani.

Soma pia: Miito yaongezeka kuhusu usitishwaji mapigano Gaza

Jana Usiku, viongozi wa Umoja wa Ulaya walitoa pia wito kama huo na kusisitiza kuwa usitishwaji huo wa muda unapaswa kusaidia kuvimaliza kabisa vita hivyo ambapo hadi sasa vimesababisha vifo vya karibu watu 32,000, idadi hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.

(Vyanzo: Mashirika)