1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Palestina zajipa miezi 9 kufikia makubaliano

31 Julai 2013

Palestina na Israel zimejipa muda wa miezi tisa kufikia makubaliano ya kumaliza mgogoro wao wa zaidi ya miongo sita sasa kupitia mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/19HaN
epa03807790 US Secretary of State John Kerry (C) speaks as Israeli Justice Minister Tzipi Livni (L) and chief Palestinian negotiator Saeb Erekat listen during a press conference after they concluded Middle East peace talks, at the State Department, in Washington DC, USA, 30 July 2013. Negotiators for Israelis and Palestinians will meet again in the region within two weeks to continue peace talks, US Secretary of State John Kerry said 30 July. EPA/MIKE THEILER
Israel und Palästina Nahost Friedensgespräche in Washington Kerry Livni ErekatPicha: picture-alliance/dpa

Akiwa amezungukwa na viongozi wa ujumbe wa mazungumzo hayo kutoka kila upande, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alikiri kutambua wasiwasi na mashaka yaliyopo, lakini akasema mazungumzo haya ya awali, yamekuwa zaidi kwenye mchakato na sio kilichomo kwenye mchakato huo.

"Si siri kwamba huu ni mchakato mgumu. Kama ungelikuwa ni rahisi, ungelikwishafanyika muda mrefu huko nyuma. Si siri pia, kwa hivyo, kwamba maamuzi mengi magumu yanatukabili kwenye siku zijazo kwa wajumbe wa mazungumzo na viongozi huku tukitafuta muafaka kwenye masuala magumu, changamano, ya kihisia na yenye umuhimu mkubwa. Nadhani muafaka ndio msingi wa jitihada zote hizi. Najua kwamba mazungumzo haya yatakuwa magumu, lakini pia najua kuwa matokeo ya kutokujaribu ni mabaya zaidi." Alisema Kerry mbele ya waandishi wa habari mjini Washington jana Jumanne.

Kerry pia ameonya kwamba na dunia haiwezi tena kurithisha kila kizazi dhamana ya kumaliza mgogoro huo ambao kuna uwezekano wa kuumaliza sasa.

Masuala muhimu lakini magumu sana

Miongoni mwa masuala muhimu kabisa kwenye mazungumzo haya ni kile kinachoitwa hadhi ya mwisho, linalojumuisha kuanzishwa kwa dola huru la Palestina, jirani ya Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, kushoto, na mjumbe maalum wa Marekani kwenye mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Martin Indyk.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, kushoto, na mjumbe maalum wa Marekani kwenye mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Martin Indyk.Picha: Reuters

Mengine ni hatima ya makaazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi, hatima ya wakimbizi wa Kipalestina na hadhi ya mji wa Jerusalem.

Masuala haya magumu ndiyo ambayo yamekuwa yakiyavunja kila mazungumzo yaliyowahi kupita huko nyuma, na kama anavyosema kiongozi wa ujumbe wa Israel kwenye mazungumzo hayo, Waziri wa Sheria Tzipi Livni, inahitajika ujasiri kuyamaliza sasa.

"Ninaamini kwamba kwa kuanzisha tena mazungumzo haya, tunaweza kujenga matumaini kwa Waisraili na Wapalestina na pia ninaamini kabisa kwamba amani kati ya Israel na Wapalestina ni kwamba maslahi ya Israel na kwa maslahi ya Palestina, maslahi ya jamii ya kimataifa, kwa hivyo tunapaswa kufanya jitihada sio tu za kuanzisha tena mazungumzo, bali pia kumaliza mgogoro." Alisema Livni akiwa njiani kutoka ukumbi wa mazungumzo.

Wakati wa Palestina huru

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo hayo, Saeeb Erakat, alisema kwamba Wapalestina wameteseka sana na hakuna anayefaidika zaidi na mafanikio ya mazungumzo haya kuliko Wapalestina wenyewe.

John Kerry (kushoto) akizungumza na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Amman, Jordan.
John Kerry (kushoto) akizungumza na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Amman, Jordan.Picha: Reuters

"Ni wakati wa Wapalestina kuishi kwa amani, uhuru na heshima ndani ya dola yao wenyewe iliyo huru."

Duru hii ya awali ya mazungumzo ilijumuisha mkutano wa faragha na Rais Barack Obama kwenye Ikulu ya Marekani na pia mazungumzo baina ya pande mbili, bila ya maafisa wa Marekani kuwepo.

Mazungumzo haya ya siku mbili, yakiwa wa kwanza ya moja kwa moja baada ya miaka mitatu ya mkwamo, yamemalizika kama ishara ya ushindi kwa Kerry, ingawa wachambuzi wengi wanayachukulia kuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman