1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya

21 Juni 2022

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett na Waziri wa mambo ya kigeni Yair Lapid wamekubaliana kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema. Huu utakuwa ni uchaguzi wa tano wa Israel ndani ya miaka mitatu.

https://p.dw.com/p/4D0LA
Israel | Jair Lapid und Naftali Bennett
Picha: JINI via Xinhua/picture alliance

Bennett alitangaza siku ya Jumatatu kuwa bunge la Israel litavunjwa na kutoa nafasi ya uchaguzi wa mapema kufanyika. Amekubali pia kwamba Waziri wa mambo ya nje Yair Lapid atachukua hatamu kama Waziri Mkuu kwa sasa. Kura inatarajiwa kufanyika bungeni wiki ijayo. Naftali Bennett amesema uamuzi wa kulivunja bunge haukuwa rahisi lakini ni muhimu kwa Israel.

Ameyasema hayo huku akihakikisha makabidhiano salama ya madaraka na kuelezea mafanikio ya serikali yake. Lapid amemshukuru Bennett akisema ameweka mbele masilahi ya nchi kuliko masilahi yake binafasi.

Lapid ameongeza kuwa hata kama  Israel itaandaa uchaguzi wake ndani ya miezi michache ijayo, changamoto za taifa haziwezi kusubiri kutatuliwa. Amesema taifa linahitaji kushughulikia masuala ya kupanda kwa gharama ya maisha, kuendesha kampeni dhidi ya Iran Hamas na Hezbollah na kupinga vikosi vinavyopanga kuibadilisha Israel kuwa nchi isiyosimamia demokrasia.

soma zaidi: Netanyahu apambana kuzuwia kuundwa serikali ya mseto

Lapid na Bennett waliunda serikali ya mseto pamoja na vyama vyengine vya kisiasa mwezi Juni mwaka 2021 hatua iliyomaliza miaka miwili ya mkwamo wa kisiasa wakati Benjamin Netanyahu aliposhindwa mara kadhaa kuunda serikali mpya.

Serikali hiyo ilijumuisha vyama vya mrengo wa kulia, kileberali na chama cha waarabu na imekuwa ikitofautiana katika masuala  kadhaa. Bennett amejaribu kusuluhisha tofauti hizo katika serikali hiyo ya mseto huku watu wakiuhama muungano huo hatua inayoupunguzia nafasi ya kuwa na wingi wa kura bungeni kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

soma zaidi: Netanyahu kuupoteza uwaziri mkuu?

Serikali hiyo ya mseto iliundwa ili kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa muda mrefu Benjamin Netanyahu ambaye kwa sasa ni kiongozi wa upinzani. Muungano wa Netanyahu umeibuka kufuatia chaguzi kadhaa kuwa chama kikubwa cha upinzani lakini bila wingi wa kura bungeni.

Uchaguzi mpya ambao ni watano nchini humo ndani ya miaka mitatu unatarajiwa kufanyika Oktoba au Novemba mwaka 2022.

Chanzo: afp