1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kufanya uchaguzi mkuu kwa mara ya tatu

12 Desemba 2019

Baada ya vyama vya siasa nchini Israel kushindwa kuunda serikali hadi muda wa mwisho kumalizika Jumatano, sasa bunge limejivunja na nchi hiyo inaingia katika uchaguzi wa tatu mkuu katika kipindi cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3Ufmk
Symbolbild - Neuwahlen in Israel
Picha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Hatua hii inampa matumaini Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anayepambana kuokoa maisha yake kisiasa akikabiliwa kashfa kubwa za ufisadi.

Machi mbili ndiyo tarehe iliyoamuliwa kwa uchaguzi ujao kufanyika. Kwa Waisraeli wengi uchaguzi huu ni jambo ambalo awali lilionekana kama lisiloweza kufanyika kutokana na gharama inayoambatana nao.

Jamii ya Israel kwa sasa imegawika pakubwa

Masaa machache kabla muda wa mwisho wa kuunda serikali hapo Jumatano, wabunge walichukua uamuzi wa kulivunja bunge wenyewe. Lakini kadri hotuba na kazi za kamati zilivyoendelea hadi usiku, wabunge walifanikiwa kupitisha sehemu moja tu ya tatu za mswada huo wa kuunda serikali. Hata baada ya muda huo wa mwisho wa kuunda serikali kupita, wabunge waliendelea kujadiliana hiyo tarehe mpya ya uchaguzi ya Machi 2.

Symbolbild - Neuwahlen in Israel
Bunge la Knesset likiwa kikaoniPicha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Ukizingatia migawanyiko iliyoko katika jamii ya Israel na kutoaminiana kwa pande mbili pinzani, matumaini ya uchaguzi mwengine kuuvunja mgawanyiko ulioko na kuleta maelewano ni madogo sana. Yair Lapid ni mbunge wa chama cha upinzani cha Buluu na Nyeupe.

"Kile ambacho awali kilionekana kama sherehe ya demokrasia, kimekuwa aibu kwa bunge hili. Uchaguzi huu una sababu tatu: rushwa, udanganyifu na kuleta kutoaminiana," alisema Yair Lapid.

Kampeni za hivi karibuni zimeshuhudia Netanyahu kudaiwa kuwachochea Waarabu walio wachache nchini humo. Lakini safari hii Waziri Mkuu huyo ambaye ndiye kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini humo atagombea chini ya wingu la kashfa iliyotangazwa mwezi uliopita. Kama waziri mkuu Netanyahu hayuko chini ya shinikizo lolote kisheria kujiuzulu na akiwa afisini anaweza kuliomba bunge limkinge katika suala la kufunguliwa mashtaka.

Netanyahu alisisitiza kwamba yeye ndiye atakayekuwa Waziri Mkuu

Kufuatia uchaguzi wa Septemba 17 chama cha Likud chake Netanyahu na kile cha Buluu na Nyeupe cha mpinzani wake Benny Gantz, wote walishindwa kupata wingi utakaowawezesha kuunda serikali ya muungano. Wote wawili walikuwa wanasisitiza kwamba hawataki uchaguzi mwengine ufanyike tena kutokana na gharama ingawa hakuna kati yao aliyekuwa tayari kulegeza msimamo katika yale aliyokuwa anayataka katika serikali ya muungano.

Israel | Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Netanyahu alikuwa anasisitiza kwamba yeye ndiye atakayehudumu kama waziri mkuu ambapo inafahamika kwamba angekuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na madai ya ufisadi yanayomkabili. Gantz alikataa kata kata kuhudumu chini ya waziri mkuu ambaye anakabiliwa na mashtaka makubwa kama hayo na akakitaka chama cha Likud kimchague mtu mwengine.

Netanyahu ambaye ameapa kupata ushindi mkubwa katika kura ijayo, amesema yeye ndiye aliye katika nafasi nzuri ya kukabiliana na kitisho cha usalama kinachoikabili Israel.