Iraq wamkumbuka Jenerali Soleimani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iraq wamkumbuka Jenerali Soleimani

Maelfu ya wafuasi wa makundi yanayoegemea Iran wameandamana katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Jenerali wa jeshi la Iran Qassem Soleimani katika shambulizi lililofanywa na Marekani.

Maelfu ya wafuasi wa makundi yanayoegemea Iran wameandamana jana katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Jenerali wa jeshi la Iran Qassem Soleimani katika shambulizi la ndege lililofanywa na Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Waandamanaji hao waliilaani Marekani na kuhimiza ulipizaji kisasi dhidi ya kifo cha kamanda huyo.

Shambulizi hilo pia lilisababisha kifo cha mshirika wa Soleimani Abu Mahdi al-Mohandes aliyekuwa naibu mkuu wa kundi la wanamgambo la Hashd al-Shaabi la nchini Iraq.

Soma Zaidi: Mauaji ya Kamanda wa Iran: Mataifa yatakaka utulivu na busara

Soma Zaidi: Jenerali Qassem Soleimani ni nani?

Waandamanaji hao walioanza kuingia mitaani tangu mapema jana, walifurika kwenye mitaa inayoelekea kwenye bustani ya Tahrir katikati ya jiji la Baghdad huku wakiwa wamebeba mabango yanayoshinikiza Marekani kuwaondoa wanajeshi wake nchini Iraq.

Irak Baghdad Proteste USA

Waandamanaji waliingia mitaa inayoelekea kwenye bustani ya Tahrir, mjini Baghdad

Siku moja kabla ya maandamano raia walitembelea kaburi alikozikwa Soleimani katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo huku wakiendelea kuhimiza kisasi dhidi ya wale waliofanya mauaji hayo. Miongoni mwao ni Mohammad Hossein aliyesema haya alipozungumza na shirika la habari la Reuters.

"Nia ya kulipiza kisasi kikubwa bado ipo na itatekelezwa wakati muafaka na viongozi wa Iran wanaufahamu wakati huo. Tunakisubiri kwa hamu kisasi hicho ili kuona maadui wetu Marekani na Israel namna watakavyojibu," alisema

Alipozungumza na waandamanaji hapo jana, mkuu wa Hashd al-Shaabi, Faleh al-Fayad naye aliapa kulipiza kisasi dhidi ya waliofanya shambulizi hilo, lakini pia akitoa mwito wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani huko Iraq.

Soleimani aliyeuawa akiwa na miaka 62 alikuwa akichukuliwa kama mmoja wa kiongozi wa kijeshi aliyekuwa na ushawishi mkubwa kabisa nchini Iraq, Syria na baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati ambako Iran pia ilikuwa na ushawishi.

Mauaji ya Soleimani yaliibua wasiwasi mkubwa wa vita.

Mauaji ya Soleimani pamoja na al-Mhandes yaliibua wasiwasi wa vita vipya vya Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Iran. Marekani ilikuwa ikimtuhumu Soleimani kwa kuandaa mashambulizi ya wanamgambo wenye mafungamano na Iran dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko kwenye ukanda huo.

Marekani yamuua afisa mwandamizi wa Iran

Hali ya hofu baina na Washington na Tehran ilichochewa zaidi na hatua ya rais wa Marekani, Donald Trump ya kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo, katika kile ambacho serikali yake ilikiita ni "kampeni kali kabisa ya shinikizo dhidi ya Iran".

Hali ya usalama iliimarishwa, na idadi kubwa ya wanajeshi wa vikosi vya usalama walipelekwa mjini Baghdad ili kuhakikisha kunakuwepo na usalama wakati wa maandamano hayo, kufuatia ahadi ya waziri wa mambo ya ndani siku ya Jumamosi kwamba kuliandaliwa mpango wa kuwalinda waandamanaji.

Usalama pia uliimarishwa kwenye maeneo yenye ulinzi zaidi mjini Baghdad, ambako kuna majengo ya balozi za nje na serikali. Eneo hilo, ambalo pamoja na kuzungukwa na teknolojia ya juu ya ulinzi, hata hivyo bado limekuwa likilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora.

Mashirika: DPAE/RTRE