Iraq na Kuwait zaingia kwenye mvutano wa mpaka wa baharini
23 Februari 2026
Mvutano kuhusu mpaka wa baharini kati ya Iraq na Kuwait ulioibuka mwishoni mwa juma umeyachochea mataifa ya kiarabu ya eneo la Ghuba kuiunga mkono Kuwait, na kuiacha Baghadad ikitowa malalamiko yake.
Mvutano huo umeibuka baada ya hivi karibuni Iraq kuwasilisha ramani na ushahidi wa kijiografia mbele ya Umoja wa Mataifa ikidai baadhi ya maeneo kwenye bahari ya ghuba ya Uajemi yako chini ya himaya yake.
Maeneo hayo ambayo ni pamoja na Fasht al-Qaid na Fasht al-Aij, kimsingi Kuwait imekuwa ikidai yako kwenye nchi yake. Qatar,Umoja wa Falme za kiarabu na Oman ambazo ni majirani wa Kuwait zimetowa matamko ya kuonesha mshikamano na nchi hiyo.
Pamoja na kwamba mahusiano kati ya Iraq na Kuwait yameimarika tangu alipoondolewa Saddam Hussein mwaka 2003 aliyeivamia Kuwait mwaka 1990, suala la mipaka ya baharini limekuwa mara zote likizusha mivutano baina ya mataifa hayo mawili.