1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatilia shaka ushiriki wa Kombe la Dunia 2026

2 Machi 2026

Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, Mehdi Taj, amesema haijulikani kama timu ya taifa ya nchi hiyo itaweza kushiriki Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/59fgH
Iran-Kandanda
Mashabiki wa kandanda wa timu ya Taifa ya Iran.Picha: AFP/Getty Images

Akizungumza na tovuti ya michezo ya Varzesh3, Taj alisema mazingira ya sasa hayatoi matumaini kuhusu maandalizi ya mashindano hayo.

"Kilicho wazi ni kwamba baada ya shambulizi hili, hatuwezi kutarajiwa kuisubiri Kombe la Dunia kwa matumaini,” alisema Taj, wakati Iran ikiendelea kubadilishana mashambulizi na Israel katika mzozo unaozidi kupanuka.

Mashambulizi hayo yaliendelea kwa siku ya pili mfululizo Jumapili, baada ya kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, tukio lililoongeza wasiwasi kuhusu mustakabali wa Jamhuri ya Kiislamu na usalama wa ukanda mzima.

Ratiba ya Iran kwenye Kombe la Dunia

Iran imepangwa Kundi G, ikiwa na mechi tatu za hatua ya makundi nchini Marekani:

Juni 15 – dhidi ya New Zealand, Inglewood, California

Juni 21 – dhidi ya Ubelgiji, Inglewood, California

Juni 26 – dhidi ya Misri, Seattle

Mashindano hayo yataandaliwa na Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.

Iran
FIFA inasisitiza kuwa kipaumbele chake ni usalama wa mashindano na kuhakikisha mataifa yote yaliyofuzu yanapata fursa ya kushiriki.Picha: GIUSEPPE CACACE/AFP/Getty Images

Hata kabla ya mzozo wa sasa, mashabiki kutoka Iran walikuwa wamekumbana na vikwazo vya kuingia Marekani kufuatia marufuku ya usafiri ya awali chini ya utawala wa Donald Trump.

Kauli ya FIFA na wadau wengine

Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) halikujibu mara moja ombi la maoni kuhusu mustakabali wa ushiriki wa Iran.

Hata hivyo, Kaweh Niroomand, mwakilishi wa Olimpiki na mchezaji wa zamani wa mpira wa wavu, amepinga vikali wazo la kuiondoa Iran kwenye mashindano hayo.

Alisema hatua kama hiyo "ni upuuzi mtupu” na haijawahi kuleta mafanikio katika historia ya michezo ya kimataifa.

Niroomand alisisitiza kuwa michezo mikubwa hutumika kuunganisha watu, si kuongeza mgawanyiko. Alionya kuwa kuifungia Iran kutaisukuma nchi hiyo katika "mwelekeo usiofaa” na kuzidi kujitenga.

Niroomand, ambaye ni mkosoaji wa serikali ya Iran, alisema wananchi wa nchi hiyo wako katika hali ya hofu na sintofahamu.

Kwa sasa, mjadala kuhusu ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia unaendelea huku FIFA ikisisitiza kuwa kipaumbele chake ni usalama wa mashindano na kuhakikisha mataifa yote yaliyofuzu yanapata fursa ya kushiriki.