1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuna matumaini ya kufikiwa muafaka wa nyuklia

13 Julai 2015

Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya wiki mbili mjini Vienna, wajumbe wanapaga kutangaza kupatikana kwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, na hivyo kuhitimisha mkwamo uliodumu kwa miaka 13.

https://p.dw.com/p/1Fxgn
Iran - Atomverhandlungen
Picha: picture-alliance/dpa

Wakati muda mwingine wa mwisho waliojiwekea ukikaribia kuisha saa sita usiku wa Jumatatu mjini Vienna, wanadiplomasia wamesema wanapanga kukamilisha na kutangaza makubaliano ya mwisho kabla ya kumalizika kwa siku hiyo.

Lakini wameonya kuwa hakuna uhakika wa hilo wakati mambo kadhaa yakiwa bado kutatuliwa. Tayari muda wa mwisho wa duru ya sasa ya mazungumzo hayo umerefushwa mara tatu, na wanadiplomasia wanasema kuna hamu ndogo ya kuyarefusha kwa mara ya nne.

Baada ya zaidi ya wiki mbili za maendeleo ya bembea, ikiwemo vitisho kutoka Marekani na Iran kujitoa kwenye mazungumzo hayo, maafisa waandamizi walianza kuelezea matumaini kuwa muafaka unakaribia kupatikana siku ya Jumapili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema mara mbili kuwa ana matumaini na kukutana tena na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif Jumapili jioni.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa mjini Vienna, Austria.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa mjini Vienna, Austria.Picha: Reuters/C. Barria

Ishara za matumaini

Baada ya mkutano huo, mawaziri wa mambo ya kigeni na maafisa wandamizi kutoka mataifa matano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani walipata chakula cha usiku cha pamoja.

Katika ishara nyingine ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na China, ambao walikuwa wameondoka kutoka kwenye mazungumzo hayo mjini Vienna wiki iliyopita, wote walirudi katika mji mkuu huo wa Austria Jumapili jioni.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius, pia alikuwa na matumaini ya tahadhari, akiwambia waandishi habari jana kuwa, "natumai hatimaye tumeingia duru ya mwisho ya mazungumzo haya marefu. Naamini hivyo."

Nchini Iran, rais Hassan Rouhani alisema makubaliano yalikuwa karibu, lakini sio kwa ukamilifu, akiyataja majadiliano kuwa yako hatua moja kufikia kilele kilichokusudiwa.

"Hata kama kazi ikiishia hapa kwa vile tuko katika hatua za mwisho za mazungumzo, sisi serikali na wapatanishi, tumetekelza majukumu yetu na kufanya kila juhudi," alisema Rouhani.

Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (katikati) akipitia nyaraka za makubaliano ya nyuklia.
Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (katikati) akipitia nyaraka za makubaliano ya nyuklia.Picha: picture-alliance/Landov/A. Mohammadi

Lengo la makubaliano

Safari ya kufikiwa makubaliano hayo imeshuhudia miaka kadhaa ya majadiliano makali. Mkataba huo unalenga kuweka udhibiti wa muda mrefu na unaoweza kuhakikiwa juu ya mpango wa nyuklia ambao Iran inaweza kuufanyia marekebisho na kutengeneza silaha za atomiki. Kwa upande wake, Iran itajipatia mabilioni ya dola kutokana na kuondolewa vikwazo vya kimataifa.

Wanadiplomasia walio karibu na mazungumzo hayo wanasema mengi ya masuala yenye utata ya utekelezaji wa makubaliano hayo yameafikiwa, lakini katika kipindi cha wiki iliyopita, masuala yaliyokuwa yameahirishwa yamesababisha mifarakano mipya.

Miongoni mwa masuala hayo ni takwa la Iran la kuondolewa mara moja vikwazo vya Umoja wa Mataifa, na msisitizo wake kuwa azimio lolote la Umoja wa Mataifa linaloidhinisha makubaliano hayo liandikwe katika namna ambayo inaacha kuzitaja shughuli za nyuklia za Iran kuwa ni haram.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe.
Mhariri: Josepha Charo