1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IOM: Zaidi ya wahamiaji 8,500 walikufa 2023 duniani

Sylvia Mwehozi
7 Machi 2024

Shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, limesema zaidi ya wahamiaji 8,500 walikufa mwaka jana duniani kote katika njia za ardhini na majini, haswa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterenia.

https://p.dw.com/p/4dFIa
Lampedusa
Wahamiaji wakiokolewa pwani ya kisiwa cha LampedesaPicha: Yara Nardi/REUTERS

Shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, limesema zaidi ya wahamiaji 8,500 walikufa mwaka jana duniani kote katika njia za ardhini na majini. Rekodi hiyo ni ya kiwango cha juu tangu shirika hilo lilipoanza kuhesabu vifo muongo mmoja uliopita.

IOM, imeongeza kwamba idadi kubwa ya vifo vya wahamiaji, ilitokea kwenye njia hatari ya kuvuka bahari ya Mediterenia. Idadi jumla ya vifo miongoni mwa wahamiaji mwaka uliopita ilipindukia asilimia 20 kuliko mwaka uliotangulia.

Soma: Mataifa tajiri yanawahitaji sana wahamiaji , asema mkuu wa IOM

Kiwango hicho pia kinajumuisha wahamiaji waliotoweka ambao mara nyingi wanajaribu kuvuka bahari na kusadikiwa kuwa wamekufa ikiwa miili yao haikupatikana. Shirika hilo pia limerekodi kiwango cha juu cha vifo vya wahamiaji vilivyotokea Afrika mwaka jana, hususan katika jangwa la Sahara, sambamba na njia ya baharini kuelekea visiwa vya Canary.