1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yarejea Afrika

Caro Robi
18 Septemba 2018

Shirika la Fedha Duniani, IMF limerejea barani Afrika. Wataalamu wanasema shirika hilo linalotoa misaada ya kifedha kwa wanachama wake limejifunza kutokana makosa yake lakini bado limeshindwa kutatua matatizo halisi.

https://p.dw.com/p/352MX
Christine Lagarde in Marokko
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Elshamy

Ongezeko la madeni ambayo yanatishia kuzifilisi nchi kadhaa barani Afrika limechochea kiu mpya kwa kurejea kufanya biashara na nchi hizo. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Angola taifa lenye utajiri wa mafuta liligeukia shirika hilo la fedha lenye makao yake mjini Washington.

Rais wa Angola Joao Lourenco anatumai kuwa mbali na nchi yake kupewa mikopo ya dharura, pia IMF itasaidia katika kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini humo.

Mataifa mengine tisa ya Afrika pia yameomba mkopo kutoka IMF ikiwemo Msumbiji, Ghana na Congo. Mpango wa IMF kwa ajili ya Afrika ulikuwa wa thamani ya dola bilioni 7.2 mwaka uliopita, hiyo ikiwa mara nne zaidi ya kiwango IMF ilizikopesha nchi za Afrika mwaka 2014.

Kuongezeka huko kwa mikopo ya IMF barani Afrika kunaibua kumbukumbu ya mzozo wa kifedha uliozikumba nchi za Afrika ambazo zilikuwa na mzigo mkubwa wa madeni katika miaka ya 80 na 90. Kipindi hicho, nchi kadhaa zilishindwa kulipa madeni yake na IMF iliombwa kutoa misaada zaidi ya dharura.

Mikopo hiyo ilikuja na masharti magumu. IMF na mshirika wake, Benki ya Dunia, waliyataka mataifa hayo ya Afrika kutekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa. Mageuzi hayo yalikuja na masharti mengine, ikiwemo kupunguza ruzuku katika sekta ya kilimo na viwanda, kupunguza kodi, kubinfasishwa kwa asasi za serikali na sera za biashara huru.

Lakini badala ya hayo kuchochea ukuaji wa kiuchumi, mageuzi hayo yalisababisha hata matatizo zaidi ya kiuchumi katika mataifa yaliyopewa mikopo na misaada na IMF. Rainer Thiele, mtaalamu kuhusu Afrika katika taasisi ya kimataifa ya uchumi iliyoko Ujerumani anasema kwa kuzingatia hayo, ni sahihi mtu kusema mipango hiyo ya kiuchumi haikufanikiwa.

Thiele anasema nchi nyingi zilikuwa na matatizo ya kulipa madeni na zilipata tabu kupata njia za kuwa na ukuaji wa kiuchumi katika mipango ya kipindi kirefu. Hata wanauchumi wa IMF walikosoa mikakati ya shirika hilo.

Katika jarida lililochapishwa mwaka 2016, wanauchumi walisema baadhi ya mageuzi yaliyotakikana na IMF katika kipindi cha nyuma yalisababisha hata pengo kubwa la ukosefu wa usawa na kuathiri ukuaji wa kiuchumi Afrika.

Hilo lilikuwa funzo kwa IMF, anasema Rainer Thiele, kwani sasa shirika hilo la fedha linatilia mkazo zaidi utawala bora na maslahi ya kijamii kuliko ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma. Wachambuzi wanasema mojawapo ya sababu za IMF kujirekebisha ni kuwa asasi hiyo na Benki ya Dunia sio pekee sasa zinazotoa misaada ya kifedha kwa serikali za Afrika.

Baadhi ya nchi hivi sasa zinaweza kujitegema kwa kutumia masoko yake ya hisa. Na kuibuka kwa mwekezaji mkubwa mwenye nguvu kubwa ya kiuchumi kumebadilisha mkondo wa kifedha Afrika. Mfadhili huyo bila shaka si mwingine bali China.

Kujitosa kwa China barani humo kumetoa fursa mpya kiuchumi na kifedha kwa mataifa mengi ya bara hilo. Mwanauchumi  Ndongo Sylla wa Wakfu wa Rosa Luxembourg kutoka Senegal anasema China inazipa nchi za Afrika fursa ya kuwa na chaguo na kuondokana na utegemezi wa IMF na Benki ya Dunia. Kingine China inaonekana kutokuwa na masharti magumu ikilinganishwa na IMF na Benki ya Dunia.

China kwa mfano haihitaji mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ili kutoa mikopo badala yake inataka kuruhusiwa kufanya biashara, kupata raslimali na kupenya masoko ya Afrika.

Mwandishi: Caro Robi/Jan Phillip Wilhelm
Mhariri: Mohammed Khelef

 LINK: http://www.dw.com/a-45479369