ICC yamtia hatiani mkuu wa zamani wa kundi la Janjaweed
6 Oktoba 2025
Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu katika uamuzi wake imemtia hatiani mkuu huyo wa wanamgambo wa kiarabu wa Sudan waliojulikana kama Janjaweed, aliyeogopwa sana wakati wake kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa wakati wa mashambulizi ya kikatili huko Darfur.
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, anayejulikana pia kama Ali Kushayb, amepatikana na hatiaya uhalifu, mauaji, mateso, ubakaji, ukandamizaji na kuwashambulia raia. yaliyotekelezwa kati ya mwezi Agosti mwaka 2003 na mwezi Aprili 2004.
Ni mara ya kwanza kwa mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu kumtia hatiani mshukiwa wa uhalifu uliotendekea katika jimbo la Darfur. Jopo la majaji watatu kwenye Mahakama ya mjini The Hague waliamua kwamba ukatili huo, ulikuwa sehemu ya mpango wa serikali ili kuuzima uasi katika eneo la magharibi mwa Sudan.
Hatia dhidi ya Ali Kushayb
Jaji Kiongozi Joanna Korner, alisoma hatia 27 katika makosa 31 yaliyomkabili Ali Kushayb na sasa anasubiri kupewa hukumu ya makosa hayo ambayo itatolewa baadae. Kutokana na makosa yanayomkabili anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Jaji kiongozi amesema Ali Kushayb,amekutwa na hatia ya uhalifu kwa kuongoza vikosi vya wanamgambo wa Janjaweed katika jimbo la Darfur ambacho kiliendesha mauaji ya mwaka 2003 hadi mwaka 2004.
Jaji Korner amesema Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, anayejulikana pia kama Ali Kushayb,"Alihimiza na kutoa maelekezo yaliyosababisha mauaji hayo, ubakaji na uharibifu mkubwa uliofanywa nakundi la Janjaweed," na ameongeza kuwa hukumu hiyo imetolewa kwa kauli moja.
Uasi wa kundi la Janjaweed
Waendesha mashtaka wamesema Abd - Al-Rahman alikuwa kamanda mkuu wa Wanamgambo wa Janjaweed wakati wa mzozo wa Darfur uliozuka pale waasi kutoka kabila la eneo la kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara walipoanzisha uasi kutokana na malalamiko ya uonevu wa serikali ya Khartoum iliyotawaliwa na jamii ya Wasudan Waarabu wakati wa utawala wa Rais aliyendolewa madarakani Omar al-Bashir na ndipo serikali hiyo iliwajibu kwa mashambulio ya ardhini na ya angani pamoja na jamii hiyo kuvamiwa na wanamgambo wa Janjaweed.
Operesheni hiyo ilijumuisha mauaji ya umati ambapo hadi watu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.7 walifukuzwa kutoka kwenye makazi yao huko Darfur kwa miaka mingi. Aliyekuwa Rais wa Sudan Omar Al-Bashir ameshtakiwa kwenye mahakama ya ICC kwa uhalifu na mauaji ya halaiki, lakini mpaka sasa hajakamatwa ili kupelekwa huko The Hague kukabiliana na sheria.
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, alifunguliwa mashataka mnamo mwaka 2022 na wakati huo alikana mashtaka yote 31 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kesi yake ilipofunguliwa Aprili 2022 na alikanusha kabisa kuwa yeye siya mtu anayejulikana na Ali Kushayb lakiani Majaji waliukataa utetezi wake huo.
Hii leo majaji wametoa uamuzi wa mashtaka 27 na hawakuamua juu ya mashtaka manne kwa sababu wameona kuwa uhalifu wa makosa hayo umejumuishwa ndani ya mashtaka mengine aliyotiwa hatiani.