1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Human Rights Watch yaitaka Uganda kumuachia mwanafunzi

Saumu Mwasimba
20 Mei 2021

Shirika la Human Rights Watch limewataka maafisa nchini Uganda kuondoa mashtaka dhidi ya mwanafunzi wa sheria Michael Muhima mwenye umri wa miaka 24 alieshtakiwa kwa kumkejeli semaji wa polisi kupitia ujumbe wa Twitter.

https://p.dw.com/p/3tfs3
Uganda Polizei
Picha: Zuma Press/Imago Images

Kijana Michael Muhima ni mwanafunzi wa sheria nchini Uganda alishtakiwa Mei 14 kwa tuhuma za kutumia lugha isiyofaa kupitia ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wa Twitter Novemba 2020 akimdhihaki msemaji wa polisi Fred Enanga. Muhima alifungwa jela na kunyimwa fursa ya kukutana au kuzungumza na familia yake na mawakili kwa kipindi cha siku tano kabla ya kuachiliwa huru kwa dhamana.

Oryem Nyeko mtafiti wa shirika la Human Rights Watch nchini Uganda anasema kwa kumshtaki Michael Muhima kutokana na ujumbe wa Twitter wa dhihaka, maafisa wa Uganda wanatuma ujumbe mbaya unaoonyesha kwamba hawaruhusu uhuru wa mtu kujieleza kwenye mitandao. Mtafiti huyo anasema badala ya kutumia kitisho cha kushtaki watu ili kuwadhibiti, maafisa wa umma wanapaswa kujifunza kukubali kukosolewa na kumulikwa, iwe ni kupitia njia za kuwakejeli au za kawaida.

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Tweet ya Michael Muhima ilitokana na kukamatwa kwa Bobi Wine na vikosi vya usalama, na maelezo yanayotolewa na msemaji wa Polisi Fred Enanga, ambayo yamekuwa yakiwashangaza raia wengi na hivyo kumgeuza kichekesho.Picha: REUTERS

Soma pia: Shirika la HRW lasema uchaguzi wa Uganda ulikumbwa na vurugu

Kwa kukukumbusha tu juu ya kisa cha kukamatwa kijana Muhima, ni kwamba mnamo Februari 5 alikamatwa nyumbani kwake mjini Kampala kutokana na ujumbe wa Twitter alioutuma Novemba 3 mwaka jana, ujumbe uliokuwa na picha ya msemaji wa jeshi la polisi Enanga, na  picha hiyo iliandamana na ujumbe uliosema hivi ''tumemkamata bwana Kyagulanyi kama sehemu ya uchunguzi wetu kuhusu kupotea kwa viatu vya bwana Amuriat''.

Ujumbe huu maana yake ni kwamba ulikuwa unamaanisha kitendo cha kukamatwa siku hiyo mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi anayefahamika zaidi kama Bobi Wine, kulikofuatiwa na hatua ya kuachiliwa huru mgombea mwingine wa urais wa upinzani Patrick Amuriat aliyeonekana akiwa hana viatu. Amuriat ni kutoka chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change FDC.

Uganda Johannesburg  Coronavirus Maßnahmen Polizei
vyombo vya usalama nchini Uganda vimekuwa vikilalamikiwa na watetezi wa haki kwa kukandamiza na kuwanyanyasa raia.Picha: Getty Images/AFP/B. Katumba

Kijana Muhima aliliambia shirika la Human Rights Watch kwamba watu wawili waliokuwa na silaha waliovaa kiraia waliodai ni wakandarasi wa kampuni ya maji ya taifa, walimnyang'anya simu yake, kumburuza na kumtia kwenye gari lililofululiza hadi ofisi ya mkurugenzi wa ujasusi wa visa vya uhalifu ambako alihojiwa kuhusu ujumbe wake huo wa Twitter.

Soma pia: Museveni lazima aimarishe haki za binadamu

Na baadae siku hiyo hiyo akapelekwa kwenye kitengo cha uchunguzi maalum huko Kireka mjini Kampala alikowekwa kizuizini kwa siku tano bila ya kuonana na familia yake wala mawakili. Aliachiwa huru kwa dhamana yapolisi siku sita baada ya kukamatwa.

Namna alivyoshughulikiwa ni kinyume kabisa na vipengele vya katiba ya mwaka 1995 ya nchi hiyo na pia sheria za kimataifa za haki za binadaamu ambapo maafisa wanatakiwa kumfikisha mtuhimiwa wa uhalifu mahakamani katika kipindi cha saa 48 na kuhakikisha anapata fursa ya kuonana na wakili na familia yake.

Lakini pia kukamatwa kwa Muhima kumekuja wakati kukishuhudiwa hatua ya watu kukamatwa ovyo na wengine kupotezwa na vikosi vya usalama vya Uganda,katika wakati wauchaguzi,kabla na baada ya uchaguzi huo uliofanyika mwaka huu 2021

Chanzo: Human Rights Watch