1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda kukaundwa serikali ya muungano Israel

18 Septemba 2019

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa Israel yanaonyesha kuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na wapinzani wake wa siasa za kidini na kizalendo wameshindwa kupata idadi ya kutosha ya wabunge katika uchaguzi wa Jumanne.

https://p.dw.com/p/3Pl9y
Bildkombo:  Benny Gantz, Avigdor Lieberman und Benjamin Netanyahu
Picha: Reuters/R. Zvulun

Hii inatoa nafasi kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano jambo ambalo huenda likauweka hatarini mustakabali wa kisiasa wa waziri huyo mkuu na kusafisha njia yake kufunguliwa mashtaka kwa madai ya ufisadi.

Matokeo ya awali yaliyotolewa na vituo vitatu vikuu vya Israel yameonyesha kuwa mpinzani mkuu wa Netanyahu Benny Gantz na chama chake cha Samawati na Nyeupe akiongoza kwa viti 32 vya ubunge mbele ya chama cha Likud cha waziri huyo mkuu kilicho na viti 30. Bunge la Israel lina wabunge 120. Huku matokeo hayo yakiwa hayaashirii kwamba Gantz ndiye atakayekuwa waziri mkuu mpya, yanaonyesha kuwa Netanyahu ambaye ameiongoza Israel kwa miaka kumi atakuwa na wakati mgumu sana kuendelea na kazi hiyo.

Matokeo ya awali Israel kawaida si ya kuaminika sana

Akiwahutubia wafuasi wake, Gantz amesema watashinikiza kubuniwa kwa serikali ya muungano huku Netanyahu naye akisema ni bora kusubiri matokeo rasmi yatakapotoka.

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa Israel kwa kawaida huwa si ya uhakika na huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutolewa Jumatano, huenda bado Netanyahu akapata ushindi, ingawa vituo vyote vitatu vimeonyesha matokeo sawa.

Benny Gantz - Blau Weiße Partei, Israel
Benny Gantz akiwahutubia wafuasi wakePicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Huku ikiwa hakuna anayeweza kupata idadi kubwa ya wabunge kati ya Netanyahu na Gantz bila uungaji mkono wa Avigdor Lieberman aliyekuwa katika serikali ya  waziri mkuu huyo, Lieberman ameebuka kama mshindi wa kweli, kwani kuna uwezekano mkubwa kwamba yeye ndiye atakayeamua atakayejumuishwa katika serikali ijayo.

Akiwahutubia wafuasi wake Lieberman alisema "tuna njia moja tu: serikali pana ya muungano na ya kiliberali itakayoundwa na chama cha Yisrael Beitenu, Likud na Smawati na Nyeupe."

Wabunge katika chama cha Gantz pia wameelezea uungaji mkono wao wa serikali ya muungano ambayo huenda ikajumuisha wadhfa wa waziri mkuu ambao utakuwa unazunguka kwa watu tofauti.

Waziri Mkuu mteule atakuwa na hadi wiki sita kuunda serikali ya muungano

Macho sasa yanaelekezwa kwa Rais wa Israel Reuven Rivlin ambaye ana jukumu la kumchagua mgombea ambaye anaamini ana uwezekano mkubwa wa kubuni serikali thabiti ya muungano. Rivlin atafanya majadiliano na vyama vyote katika siku chache zijazo ili kusikiliza mapendekezo yao kabla kufanya uamuzi wake.

Israel Parlamentswahlen Präsident Rivlin
Rais wa Israel Reuven Rivlin akipiga kuraPicha: picture-alliance/Photoshot/Jini

Baada ya hapo waziri mkuu mteule atakuwa na hadi wiki sita kuunda serikali ya muungano. Iwapo hilo halitofanyika Rivlin atatoa nafasi kwa mgombea mwengine aunde serikali katika kipindi cha siku ishirini na nane na iwapo hilo nalo litashindikana basi kutaitwa uchaguzi mwengine mkuu. Rivlin amesema atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa haifikii hatua hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza wameonyesha hisia tofauti kuhusiana na uchaguzi huo wa Israel. Saeb Erakat ambaye ni afisa mkuu wa Palestina anayeongoza majadiliano na ambaye pia ni msaidizi wa karibu wa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ameeleza matumaini yake kwamba serikali mpya ya Israel huenda ikatafuta amani na Wapalestina.