1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Wasichana waliojifungua waacha shule Msumbiji

19 Februari 2024

Wasichana wajawazito au wenye watoto nchini Msumbiji, hulazimika kuacha shule kutokana na kukabiliwa na vikwazo na kutopata usaidizi wa kutosha kutoka shuleni hasa katika moja ya nyakati hatari zaidi katika maisha yao.

https://p.dw.com/p/4cZrL
Haki na Sheria l Msichana baada ya kujifungua
Msichana akimpakata mtoto wake.Picha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP/picture alliance

Hayo ni kulingana na ripoti iliyotolewa siku ya Jumatano na shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch. 

Shirika la Human Rights Watch (HRW) limeelezea katika ripoti yake yenye kurasa 52 kuwa wasichana wenye watoto mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa na ukosefu wa usaidizi na malazi ambavyo hupelekea kuwa vigumu kutimiza majukumu yao ya shuleni na malezi ya watoto wao.

Elin Martinez, mtafiti mkuu wa haki za watoto katika shirika hilo la HRW amesema vikwazo hivi hupelekea wasichana wengi, ambao ni wajawazito au wenye watoto kuacha shule kabla ya kumaliza elimu yao ya msingi. kadhalika, ukosefu wa elimu ya bure husababisha wasichana wengi kutoka kaya maskini kuacha shule.

Soma pia:Uganda: Ruksa wasichana wadogo kutumia uzazi wa mpango

HRW imeitaka Msumbiji kupitisha kanuni zinazoweza kutekelezwa kisheria ili kuhakikisha haki ya wasichana ya kupata elimu wakati wa ujauzito na wanapojifungua, na pia kutoa elimu ya kina kuhusu elimu ya ngono na kuwepo pia vituo vya kulelea watoto.

Gharama kubwa ya elimu inahusisha ada, malipo ya uandikishaji, sare za shule na gharama zingine zisizo za moja kwa moja kama vile gharama ya usafiri.

Wachambuzi: Wasichana walitengwa kisheria

Mwaka 2003, serikali ya Msumbiji ilipitisha sheria ambayo iliwaamuru maafisa wa elimu kuwahamisha wasichana wajawazito na wenye watoto kwenye shule za usiku.

Haki na Sheria | Wasichana na watoto wao
Wasichana waliopata watoto mapema wakifanya wakiwa na watoto waoPicha: Miriam Kaliza/DW

Agizo hili lilianisha kutengwa kwa wanafunzi hao katika mfumo rasmi wa elimu ya kitaifa, na hivyo kuwanyima wanafunzi hao haki ya kuendeleza elimu yao katika shule za msingi na sekondari.

Kutokana na shinikizo la mashirika ya kiraia nchini Msumbuji, serikali mnamo mwaka 2018 ilibatilisha hatua hiyo ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wajawazito na kina mama, lakini hadi leo hii walimu na hata wanafunzi hawana maelekezo yaliyo wazi kuhusu kulinda haki yao ya elimu.

Soma pia:Kiwango cha mimba za utotoni nchini Uganda bado kiko juu

Human Rights Watch inasema licha ya hatua hiyo ya serikali, Msumbiji bado inahitaji kukabiliana na vikwazo vikubwa vya kimfumo na kijamii wanavyokabiliana navyo wasichana ili kusalia shuleni.

Shirika hilo limesema pia kuwa liligundua kwamba baadhi ya walimu na mamlaka za shule waliwaelekeza wanafunzi katika shule za usiku kutokana na unyanyapaa, mazoea ya kibaguzi yaliyopo au mwongozo usio rasmi kutoka kwa maafisa wa elimu.

Msumbiji ina rekodi mbaya linapokuja suala la elimu ya wasichana. Inashikilia nafasi ya tano duniani kwa kushuhudia ndoa za utotoni huku kiwango cha mimba za utotoni pia kikiwa juu zaidi kuliko mataifa yote ya mashariki na kusini mwa Afrika.

Inaarifiwa kuwa angalau msichana mmoja kati ya kumi nchini Msumbiji  hupata mtoto kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.

Kurunzi Wanawake: Tatizo la mimba za utotoni Uganda