HRW: Polisi Kenya, imewaua raia kinyume cha sheria | Masuala ya Jamii | DW | 03.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

HRW: Polisi Kenya, imewaua raia kinyume cha sheria

Ripoti iliyochapishwa na shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema jeshi la polisi liliwauwa wanaume na vijana wa kiume wasiopunguwa 21 katika maeneo ya kipato cha chini Nairobi, Kenya.

Waliwaua kwa madai ya uhalifu ambayo hayakuthibitishwa kisheria. 

Mauaji hayo ambayo hayakuzingatia sheria ni sehemu tu ya tatizo pana la polisi kutumia nguvu kubwa na bila ya kufuata sheria chini ya mwamvuli wa kudumisha sheria na utulivu katika maeneo ya mabanda kwenye mji huo mkuu wa Kenya, lakini wakishindwa kuendana na sheria inayosema mauaji yote yanayofanywa na polisi yanatakiwa kuripotiwa na kuchunguzwa ili watakaokutwa na makosa ya mauaji kinyume cha sheria washitakiwe.

Kulingana na shirika hilo la Human Rights Watch, tangu mwaka 2018, polisi wa Nairobi waliwapiga risasi na kuwaua, tena kinyume cha sheria takriban watu 21, wanaume na vijana wa kiume waliodaiwa kuwa wahalifu katika maeneo la Dandora na Mathare pakee.   

Wanaharakati wa haki za binaadamu kwenye maeneo hayo wanaamini kwamba polisi iliwauwa watu wengi zaidi kinyume cha sheria mwaka uliopita, kwa kuzingatia visa wanavyovifahamu na vile ambavyo viliripotiwa na vyombo vya habari.

Chini ya sheria ya kimataifa na ya Kenya, polisi anatakiwa kutumia nguvu pale tu wanapolazimika ama kunapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Afrika Obdachlosigkeit - Nubians in Kenia (picture alliance/AA/R. Canik)

Inadaiwa mauaji hayo yalifanyika kwenye mitaa ya mabanda iliyoko Nairobi, Kenya

Human Rights Watch inaitaka serikali ya Kenya kuwatia hatiani polisi wanaohusika na mauaji.

Human Rights Watch iliwahoji watu 35, ikiwa ni pamoja  na mashuhuda, wanafamilia na wahanga wa visa hivyo katika kipindi cha mwezi Aprili na Mei, lakini pia baadhi ya maafisa wa polisi na msemaji wa jeshi hilo jijini Nairobi. Lakini pia limeshirikiana kwa karibu na mashirika ya haki za binaadamu ya Dandora na Mathare katika kuwabaini wahanga na familia zao.

Mfanyabiashara mmoja, ambaye pia ni mtoa taarifa kwa jeshi la polisi ameliambia shirika hilo kwamba polisi wana orodha ya watu wanaopanga kuwaua.

Vyombo vya habari vya Kenya mara kadhaa huripoti mauaji hayo kama sehemu ya utekelezaji wa sheria katika maeneo hayo ya kipato cha chini. Oktoba 2018, gazeti la Star liliripoti kwamba polisi wa Dandora, Mathare na Majengo waliwaua watu 17 katika kipindi cha siku 7. Mwezi huohuo gazeti la Daily Nation liliripoti watu 101 waliouawa jijini Nairobi na zaidi ya 180 kote nchini humo katika kipindi cha miezi 9. Hata hivyo havikuweka wazi iwapo mauaji hayo yalikuwa ya haki.

Msemaji wa jeshi la polisi la Kenya Charles Owino amesema hana taarifa kamili kuhusu mazingira ya uchunguzi huo, huku akitoa mwito kwa taasisi inayoangazia utendaji kazi wa polisi, IPOA kuchunguza mauaji hayo. Amesema afisa yoyote anayekiuka sheria atawajibishwa. 

 

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com