1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yaitaka Iran kuacha kushambulia mataifa ya Ghuba

14 Machi 2026

Kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas limetoa wito leo kwa mshirika wake Iran kusitisha mashambulizi dhidi ya mataifa jirani ya Ghuba.

https://p.dw.com/p/5AOWS
 Dubai 2026 | shambulizi la Iran
Moshi wafuka kutokana na shambulizi la Iran mjini Dubai mnamo Machi 1, 2026Picha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa yake, kundi hilo limesema Tehran ina haki ya kujibu mashambulizi ya Israel na Marekani, lakini imeitaka kujiepusha na mashambulizi dhidi ya nchi jirani.

Hamas pia imetoa wito kwa nchi za Ghuba kushirikiana ili kukomesha mashambulizi hayo na kudumisha uhusiano wa kindugu miongoni mwao.

Tangu kuanza kwa vita vya Israel na Marekani dhidi ya Iran, mataifa kadhaa ya Ghuba yamekuwa yakishambuliwa na makombora na droni za Iran.

Kwa miongo kadhaa, Iran imeisaidia Hamas kifedha na kijeshi katika harakati zake huku kundi hilo likiwa pia na uhusiano wa karibu na Qatar.

Wiki mbili zilizopita, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran, huku mzozo huo ukienea katika eneo pana la Mashariki ya Kati.

Tehran imelipiza kisasi kwa mashambulizi dhidi ya Israel pamoja na kambi za jeshi la Marekani na vituo vya mafuta na gesi asilia katika mataifa ya Ghuba yanayoshirikiana na Washington.