1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ataka usitishaji haraka mapigano Syria

Sekione Kitojo
26 Februari 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres ametaka kutekelezwa  mara  moja  kwa  azimio la baraza la Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa linalotaka  kusitishwa mapigano kwa  muda  wa  siku  30  nchini  Syria.

https://p.dw.com/p/2tKlF
Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel Guterres
Picha: Reuters/T. Negeri

Wakati huo  huo  raia  walionaswa  katika  mapigano  makali nchini Syria  bado  wanasubiri  misaada  ya  chakula  na  madawa leo Jumatatu  baada  ya  majeshi ya  serikali  kushambulia eneo la Ghouta mashariki licha  ya azimio la Umoja wa mataifa  kutaka  kusitishwa  mapigano. 

Katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  mataifa Antonio Guterres amesifu baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  mataifa kuidhinisha  azimio  hilo Jumamosi  iliyopita  baada  ya siku  kadhaa  za  mjadala  uliochukua  muda  mrefu, lakini amesisitiza  kwamba  azimio  la  Baraza  hilo la  Usalama litakuwa  tu  na  maana  iwapo  litatekelezwa kwa  dhati, na ndio  sababu  amesema  anatarajia azimio  hilo litatekelezwa  na  kuendelezwa.

USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa/M. Rajmil

Mkuu  wa  sera  za  mambo  ya  kigeni  wa  Umoja  wa Ulaya  Federica Mogherini ametoa  wito  akitaka kutekelezwa  mara  moja  makubaliano  ya  kusitisha mapigano  nchini  Syria.  Mogherini  amesema  kabla  ya kikao  cha  mawaziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Umoja  wa Ulaya  mjini  Brussels  kwamba  azimio  la  Umoja  wa Mataifa ni  hatua  muhimu na  inayotia  moyo, lakini ni hatua  ya  kwanza.

Watu zaidi ya 500 wauwawa

Zaidi  ya  watu 500  wameuwawa  katika  mashambulizi makubwa  ya  majeshi  ya  rais Bashar al-Assad mbayo yameshambulia  eneo  hilo  la  Ghouta lililoko  ukingoni mwa  mji  mkuu  Damascus kwa  wiki  sasa.

Baada  ya  siku  kadhaa  za  mivutano  ya  kidiplomasia, baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa siku  ya Jumamosi  liliidhinisha  azimio  linalotaka  kusitishwa mapigano kwa  muda  wa  siku  30 nchini  Syria, bila kuchelewa, kuruhusu upelekaji wa misaada na  kuwaondoa wagonjwa  na  waliojeruhiwa. Mkaazi  mmoja  wa mji wa Damascus  hata hivyo ameonesha  shaka  kuhusiana  na makubaliano  hayo  ya  kusitisha  mapigano.

Syrien Angriffe auf Ost-Ghuta
Majengo yaliyoharibiwa kwa vita katika mji wa douma, Ghouta mashariki nchini YsriaPicha: Reuters/B. Khabieh

"Usitishaji huu wa mapigano ni sawa  na mwingine uliopita na tutaona utavunjwa na  kukiukwa. Hiki  ni  kichekesho ambacho hatupaswi  kukiamini, na hii ni  ya  zamani, iwapo inarudiwa sisi  ndio tunashambuliwa. Huoni watoto, watu wazima, wanawake na wanafunzi? Nani tunapaswa kumsikitikia, kwa  wapinzani?, Balozi wa  Syria  katika Umoja  wa  mataifa al-Ja'afar, Mungu  amlinde , alisema kuna watu  milioni  nane ambao  hatuwajali, lakini tunajali tumbuli 700."

Shirika  linaloangalia  haki  za  binadamu  nchini  Syria, limesema kiasi  ya  raia 14  ikiwa  ni  pamoja  na  watoto wameuwawa  katika  mashambulizi  ya  anga  jana Jumapili,  na  kufikisha  jumla  ya  watu  waliouwawa  kuwa 530, miongoni  mwao  zaidi  ya  watoto 130.

Mfanyakazi  wa  shirika  la  kutoa  misaada  mjini  Douma, alinukuliwa  na  shirika  la  misaada  la  Uingereza  la  Save the  Children, akisema  kusita  kwa  muda  kwa mashambulizi  ya  mabomu  kumesaidia  watu  kujitokeza baada  kujificha kwa  muda  wa  wiki  nzima.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Josephat Charo