Ghadhabu za waislam dhidi ya uamuzi wa rais wa Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ghadhabu za waislam dhidi ya uamuzi wa rais wa Marekani

Waumini wa kiislamu ulimwenguni wanaandamana kulaani uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Mapambano makali yameripotiwa na zaidi yanasuibiriwa mnamo ijumaa ya kwanza tangu rais wa Marekani alipotangaza uamuzi wake wa kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa la Israel. Wapalastina waliojaa ghadhabu sawa na waarabu na waislam kutoka kila pembe ya dunia wameteremka majiani kulaani uamuzi huo.

Wauguzi katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina tangu Gaza mpaka Hebrone wanasema polisi  wa Israel wametumia risasi kuwatawanya waandamanji. Dazeni kadhaa za wapalastina wamejeruhiwa. Wizara ya afya ya Palastina imesema katika ripoti yake hivi punde bwana mmoja amepigwa risasi na kufa karibu na mpaka wa Gaza. Vikosi vya usalama vya Israel vimesema vimewatawanya wapalastina kadhaa waliokuwa wakijaribu kuandamana, wengine wakibeba mabango yenye picha za Trump karibu na  mji mkongwe wa Jerusalem yanakokutikana maeneo matukufu kwa waumini wa dini zote tatu kuu, Waislam, wakristo na wayahudi. Vikosi vya polisi vimeimarishwa katika eneo lote la mji wa Jerusalem na katika mji mkongwe.

Mjini Cairo pia maandamano yameripotiwa baada ya sala ya ijumaa. Mbunge wa zamani Kamal Abu-Eita anatahadharisha dhidi ya madhara ya kutangazwa mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na kusema "Rais wa Marekani,Trump anabidi atambue kwamba Palastina iko ndani ya nyoyo za waarabu wote, za waislam wote na ndani ya moyo wa kila mtu anaependa amani ulimwenguni. Anabidi atambue kwamba hana haki ya kuwapa waisrael haki ambazo sizake. Jerusalem ni mji unaokaliwa kwa mabavu."

Mapambano kati ya wapalastina na vikosi vya usalama vya Israel

Mapambano kati ya wapalastina na vikosi vya usalama vya Israel

Jerusalem ni mji wa waarabu,wanasema waandamanaji wa Jordan

Maandamano yameripotiwa pia  nchini Jordan, Iran, Pakistan, Malaysia, Indonesia na katika nchi nyengine kadhaa za kiislam. Nchini Jordan mamia wamepaza sauti wakidai "Jerusalem ni ya waarabu.

Viongozi wa Ufaransa na Libnan wanaokutana mjini Paris wameonya uamuzi wa Marekani kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel unatishia usalama wa eneo lote la mashariki ya kati.

 Wakati huo huo Jibril Rajoub, afisa wa ngazi ya juu wa FATAH  akihojiwa na  Televisheni ya al Arabiya amesema viongozi wa Palastina wanapaswa wasikubali kukutana na makamo wa rais wa Marekani Mike Pence atakapofika ziarani katika eneo hilo baadae mwezi huu.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com